WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wamekaa kimya kwa muda wa dakika
moja kumkumbuka aliyekuwa Rais wa awamu ya pili ya Zanzibar, Aboud Jumbe
Mwinyi aliyefariki mwezi uliopita ambaye alikuwa muasisi na mwanzilishi
wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, ambacho ni chombo cha kutunga
sheria.
Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid alisoma wasifu wa
Mzee Jumbe na kusema atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika kukuza
na kuimarisha demokrasia, ikiwemo kuanza kwa harakati za kutungwa kwa
katiba ya kwanza ya Zanzibar ya mwaka 1979 pamoja na kuanzishwa kwa
Baraza la Wawakilishi katika mwaka 1980.
“Huo ndiyo mchango mkubwa wa Jumbe katika harakati za demokrasia
Zanzibar ambayo ilifanya kuanzishwa kwa Baraza la Wawakilishi ambapo
yeye binafsi aliita ndiyo ngome ya wananchi,” alisema.
Maulid alisema mchango mkubwa wa Jumbe ni kuchangia kuzaliwa kwa
Chama Cha Mapinduzi(CCM) mwaka 1977 baada ya kuvunjwa kwa vyama vya Tanu
na ASP na kuzaliwa chama kipya ambacho kimefanikiwa kushika hatamu ya
uongozi hadi leo.
Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
pamoja na Makamu wa rais wa Jamhuri ya Muungano kuanzia mwaka 1972 hadi
mwaka 1984 wakati alipolazimika kujiuzulu nyadhifa zote kwa sababu za
kuchafuka kwa hali ya kisiasa Zanzibar.
Chanzo :swahiba media


0 comments :
Post a Comment