Msemaji wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Christopher Ole Sendeka amemtaka Rais John Pombe Magufuli kukagua akaunti za kamati za bunge na viongozi wake hususani zile zinazosimamia mashirika na taasisi za umma zilizotajwa kuwa na ufisadi.
Ole Sendeka ametoa wito huo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika makao makuu ya CCM yaliyopo Lumumba, jijini Dar es Salaam.
Pia amemsisitiza Rais Magufuli kuendelea kukagua taasisi, mashirika ya umma pamoja na wizara ili kubaini wanaotumia fedha za serikali kinyume cha sheria.
“Serikali iendelee kukagua mashirika na wizara ili waliotumia fedha kinyume cha sheria na taratibu wachukuliwe hatua za kisheria kwa kupelekwa mahakamani,” amesema.
Ameongeza kuwa “Wakati umefika kwa serikali ya CCM kutoshughulikia maafisa masuhuli wa mashirika na taasisi hizo pekee, bali waangalie na akaunti za viongozi wa kamati za bunge ambao walikuwa wanasimamia taasisi na mashirika yaliyokutwa na ufisadi,” amesema.
Licha ya hayo, Ole Sendeka amedai kuwa kuna baadhi ya matajiri wanaokwepa kulipa kodi huutumia utajiri wao kushawishi baadhi ya vijana kuikejeli serikali pamoja na kuvishawishi vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi kuandika makala zenye lengo la kuichafua serikali.
“Tunajua kwamba hawana ujasiri wa kusimama na kusema wanalazimishwa kulipa kodi, baadhi yao wametubu na kufuata kanuni na sheria za ulipaji kodi, lakini wengine wanatumia ukwasi wao katika kushawishi baadhi yavyombo vya habari vya nje na ndani ya nchi kuandika makala za kuikejeli na kuichafua serikali,
“Kumekuwepo na usambazaji wa taarifa za upotoshaji zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa kupitia katika baadhi ya vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, makala hizo zinalenga kukejeli, dhihaki, kubeza na kuikatisha tamaa serikali ili ishindwe kutekeleza majukumu yake,” amesema.
Amesema licha ya kejeli hizo, serikali itaendelea kuwa imara na kwamba utendaji kazi wake hautafutika katika mioyo ya wananchi kwa sababu ya kelele za baadhi ya watu.
“Serikali ya Magufuli haina gia ya kurudi nyuma itaendelea kusonga mbele,” amesema.
Hata hivyo, Ole Sendeka amesema CCM inatarajia kutoa taarifa za mafanikio na utekelezaji wa ilani yake katika kipindi cha mwaka mmoja kabla ya Novemba 5, 2016.