*Ni kwa ajili ya kuzuia migogoro ya mipaka na wanavijiji
*Aagiza TAMISEMI isimamishe usajili wa vijiji kuanzia leo
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa miezi na siku tisa kwa Wakuu wa Mapori ya
Hifadhi za Misitu kuhakikisha wanaweka mawe ya alama (beacons) kwenye
mipaka yao ili kuepusha migogoro na wanavijiji wanaowazunguka.
Ametoa
agizo hilo jana jioni (Jumatatu, Novemba 21, 2016) wakati akizungumza
na Watendaji Wakuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii na Wakuu wa Mapori
ya Hifadhi za Misitu nchini katika kikao alichokiitisha kwenye ukumbi wa
Ofisi ya Waziri Mkuu mjini Dodoma.
“Tatizo
la migogoro baina ya wafugaji, wakulima na kamati za ulinzi na usalama
za mikoa na wilaya ni lazima lifanyiwe kazi. Mkitoka hapa rudini katika
maeneo yenu mkawaambie wananchi mipaka yenu iko wapi. Ninyi mnatambua
mipaka yenu iko wapi kwa hiyo waelewesheni wananchi kwa kuweka alama,” alisema.
“Wakati
Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli akizindua bunge tarehe 20 Novemba, 2015
aliwapa maeneo makuu matatu ambayo ni kuanisha mipaka, kupambana na
ujangili na kukusanya mapato. Alizungumzia suala la mipaka kwa sababu
iliyopo haieleweki, mkiulizwa mnajibu kuna buffer zone. Hivi mwananchi
wa kawaida anajua buffer zone ni nini?,” alihoji.
“Sasa
ninawapa muda hadi Januari 31, 2017 kazi ya kuweka beacons kwenye
hifadhi zote za misitu iwe imekamilika. Kila pori nenda mkatengeneze
alama zenu kama TANROADS walivyofanya. Kaeni mpige hesabu ni kiasi gani
cha saruji na kokoto kinahitajika. Tutarudi hapa Dodoma kupeana taarifa
ya utekelezaji. Katibu Mkuu niletee taarifa ya kila mkoa na wilaya kuna
mapori mangapi tutakutana hapahapa kupeana mrejesho,” alisisitiza.
Alisema
kama TANROADS waliweza kuweka alama za barabarani kwa nchi nzima ni kwa
nini Wizara ya Maliasili na Utalii imeshindwa kuchukua hatua kama hizo.
“Ni lazima tuweke hizo alama kila katika pori lake, tusipofanya hivyo, migogoro hii itaendelea,” alisema.
“Nendeni
mkaweke alama za mipaka mkishamaliza sasa muwaeleze wananchi ni umbali
wanapaswa waache kutoka kwenye hizo alama zenu na muwaelimishe kwamba
hiyo ndiyo buffer zone. Suala la beacons ni serious na ninatarajia
nikute hizo beacons kwenye maeneo yenu”
“Kila
mmoja anayo fursa ya kuitisha mkutano na wananchi na kuwaelimisha
kuhusu umuhimu wa kuwa na mapori ya akiba. Pandeni kwenye majukwaa,
muelezee mipaka hiyo mipya na wananchi watawaelewa kwa sababu mwenye
dhamana ya kwanza katika kutoa elimu hii ni wewe Mkuu wa Pori,” alisistiza.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema kuanzia leo Ofisi ya Rais TAMISEMI haina budi
kusitisha usajili wa vijiji hadi zoezi la kuweka alama kwenye mipaka
mapori ya hifadhi za misitu litakapokalimika.
“Kuanzia
leo ninasimamisha zoezi la usajili wa vijiji unaofanywa na TAMISEMI
hadi wizara ya Maliasili na Utalii ikamilikshe zoezi la kuainisha na
kuweka alama kwenye mipaka mapori ya hifadhi za misitu. Tusipofanya
hivyo tutaendelea kuwa na Taifa la walalamikaji,” alisema huku akishangiliwa na watendaji hao.
“Wakuu
wa mapori tambueni ni vijiji vingapi ambavyo Serikali ilifanya makosa
na kuvisajili wakati viko ndani ya hifadhi na vijiji vingapi bado
havijasajiliwa. Pia onyesheni ni vijiji vingapi ambavyo ni hatarishi,” alisema.
Wakati huo huo, Waziri
Mkuu amemtaka Mkurugenzi wa Idara ya Utalii katika wizara hiyo, Bw.
Zahoro Kimwaga pamoja na Bodi ya Utalii nchini wabadilike na kuanza
kufanya kazi kibiashara zaidi.
“Mkurugenzi
wa Utalii na Bodi yako ya Utalii bado hamjajitangaza vya kutosha.
Promosheni ya utalii hapa nchini bado haitoshi na mgeweza kuoata mapato
makubwa zaidi kwa kujitangaza. Mabango ya barabarani yamejaa matangazo
ya Vodacom na Airtel badala ya kuwa na picha za wanyama ili kila mtu
akiona atamani kwenda mbugani,” alisema.
“Tumieni
mabango ya kieletroniki (electronic screens) kurusha picha za wanyama.
Mfano pale nje ya uwanja wa Taifa, au uwanja wa ndege hata kwenye njia
kuu za mikoani wekeni mabango ya iana hiyo. Ombeni vipindi kwenye
televisheni nyingine, kile cha TBC1 peke yake hakitoshi,” alisisitiza.



0 comments :
Post a Comment