Msimamo wa Trump Kuitafuna Afrika ..!!!


SIKU chache baada ya Rais wa 45 wa Marekani, Donald Trump ‘kuwatumbua’ mabalozi wa nchi hiyo duniani, wasomi wameibuka na kusema hilo ni suala la kawaida, lakini kama misaada itasitishwa Bara la Afrika litaathirika zaidi kuliko mataifa mengine.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema Marekani ni moja kati ya nchi zinazochangia zaidi, hivyo bila shaka wanufaika wataathirika, ukiwamo Umoja wa Mataifa (UN) wenyewe.

Alisema kama Rais Trump ataendelea na msimamo wake wa kusitisha misaada kupitia UN, wafanyakazi wa Umoja huo watakosa ajira kwa vile ni kati ya wanufaika namba moja.

“Lazima tufahamu uchumi wa wanufaika wa misaada wataathirika na wengine kukosa ajira, hilo litakuwa anguko la mwaka,” alisema.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CHADEMA, Profesa Mwesiga Baregu alisema hatua iliyochukuliwa na Rais Trump ni ya kawaida ili kujipatia fursa ya kupanga safu mpya ya uongozi.

Alisema lakini kutokana na falsafa ya Rais huyo amekuja kubana matumizi kwa nchi tegemezi, ikiwamo kutoa misaada ya fedha kwa ajili ya bajeti na misaada mingine ya kiuchumi.

“Nchi zilizotegemea misaada kutoka Marekani zinapaswa kujiandaa, inawezekana misaada itakayotolewa isiwe kwa kiwango kilichotarajiwa,” alisema.

Wakili wa Kujitegemea, Alex Masaba alisema kitendo cha kusimamishwa kwa mabalozi wa mashirika ya kimataifa kimetokana na kusuasua kwa UN katika utendaji wake.

Alisema hiyo itakuwa njia bora kwa Rais Trump kuionesha Dunia kuwa hafurahishwi na utendaji wa taasisi hiyo ya kimataifa na kutaka kubadili muundo wa kiutawala.

“Kila mtawala anapoingia lazima afanye mabadiliko ya uongozi ili kutekeleza majukumu yake kuendana na kasi ya Serikali husika,” alisema.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Deus Kibamba alisema hakuna kitu kipya alichofanya Rais Trump kwa vile huo ni utaratibu wa Marekani.

Alisema baada ya chama cha Damocratic kumaliza muda wake na Republican kutangazwa mshindi, mabalozi wote walikosa sifa ya kuendelea na nyadhifa zao.

“Unajua Trump alipotangazwa kuwa Rais, mabalozi waliokuwa wakiwakilisha nchi hiyo walifunga virago kurudi kwao, hivyo hilo si jambo jipya kwa Wamarekani, bali ni utamaduni wao,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment