Bunge
la Gambia limerefusha utawala wa Rais Yahya Jammeh kwa miezi mitatu
baada ya kiongozi huyo kutangaza hali ya hatari katika taifa hilo na
ikiwa imebaki siku moja tu kabla ya muhula wake kumalizika rasmi .
Tangazo
la bunge kurefusha madaraka ya rais Jammeh kwa miezi mitatu yanafuatia
amri iliyotangazwa na kiongozi huyo kutokana na kile alichokiita ni
kuingiliwa kwa kiasi kikubwa na mataifa ya kigeni katika uchaguzi wa
Desemba mosi na mambo ya ndani ya Gambia.
Kwa
tangazo hilo wananchi wa Gambia "wamepigigwa marufuku kufanya matendo
yoyote ya kutoheshimu sheria, kuchochea ghasia na kuvuruga amani".
Hali ya hatari
Kupitia Televisheni ya taifa, Rais Jammeh amesema kuwa, "Mimi
Sheikh Profesa Alhaji Dr Yahya A.J.J. Jammeh rais wa Jamhuri ya
kiislamu ya Gambia na Amiri Jeshi mkuu, natangaza hali ya hatari kwa
nchi nzima ya Gambia kama hali ilivyo na ikiwa itaendelea inaweza
kusababisha hali ya hatari kwa umma", amesema Jammeh.
Chini
ya katiba ya Gambia hali hiyo ya hatari itadumu kwa kipindi cha siku 90
ambapo bunge la nchi hiyo tayari limepitisha azimio la kuithibitisha na
hiyo inamaanisha rais Jammeh atasalia madarakani kwa kipindi cha miezi
mitatu.
Marekani
imemtaka rais Jammeh ambaye ameitawala Gambia kwa miaka 22 kuachia
madaraka na kumkabidhi rais mteule Adama Barrow ambaye yupo nchini
Senegal anakopanga kubakia hadi hapo kesho siku ya kuapishwa kwake.
Jumuiya
ya kiuchumi ya mataifa 15 ya magharibi mwa Afrika ECOWAS nayo imetoa
wito kwa kiongozi huyo kuheshimu matokeo ya uchaguzi na kuondoka
mamlakani, wito unaoungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa, na Umoja wa Afrika na wengine.
Jammeh amekataa ujumbe wa viongozi wawili wa ngazi ya juu wa Afrika Magharibi ambao walimtolea wito wa kuondoka.
Raia wa nje waondolewa
Kutokana
na tangazo hilo, mataifa ya kigeni yamesema yatawaondoa raia wake,
wizara ya mambo ya kigeni ya Uingereza imeandika katika tovuti yake kuwa
"uwezekano wa kuingilia kijeshi na usumbufu wa kiraia ni mkubwa",
tahadhari ambayo imeungwa mkono na Uholanzi kupitia mitandao ya kijamii
ikiwataka raia wake kuepuka kusafiri labda ikiwa ni kwa umuhimu.
Wakala
wa utalii wa Uingereza Thomas Cook kupitia taarifa yake imesema
inapanga kuwaondoa wateja wake watalii wapatao 3500 kupitia uwanja wa
ndege wa Banjul katika masaa 48 yajayo.
Tayari
mawaziri wanne katika serikali ya rais Jammeh wamejiuzulu wiki hii
ambao ni waziri wa fedha, waziri wa biashara, waziri wa utalii, na
waziri wa mambo ya nje, na kuungana na waziri wa mawasiliano ambaye
aliachia wadhifa wake wiki iliyopita na sasa yuko Senegal.
Raia nchini humo wameendelea kukimbia kutoka Gambia wakielekea nchi jirani za Senegal, Guinea-Bissau na Guinea.
Taarifa
kutoka Nigeria zinasema maandalizi ya kuwapeleka wanajeshi kadhaa mjini
Dakar Senegal yamekamilika hali inayohusishwa na kile kinachojiri
nchini Gambia.
Chanzo: DW



0 comments :
Post a Comment