Kaimu Meneja Mawasiliano wa
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Bw. Semu Mwakyanjala akizungumza
na waandishi wa Habari kuhusu ulaghai kupitia simu za mkononi unaofanywa
na matapeli katika kipindi hiki. Kulia ni Afisa Uhusiano wa TCRA Bi.
Mabel Masasi
Baadhi ya waandishi wa Habari wakifuatilia mkutano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) leo Jijini Dar es salaam.
(Picha na Frank Mvungi-Maelezo).
…………..
Fatma Salum- MAELEZO
Serikali kupitia Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa tahadhari kwa watumiaji wa huduma za
mawasiliano nchini kuwa makini na utapeli unaofanywa kupitia simu za
mkononi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini
Dar es salaam na Kaimu Meneja Mawasiliano kutoka Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) Bw. Semu Mwakyanjala wakati akizungumza na waandishi wa
habari.
Semu alisema kuwa kuna ongezeko la
matapeli wanaoghushi utaratibu wa mawasiliano na kuwalaghai watu kutuma
pesa kwa simu za mkononi hivyo Mamlaka na vyombo vya usalama
vinashughulikia suala hilo.
“Usitekeleze maagizo yoyote
yanayohusu fedha kwa mawasiliano ya simu hata kama yanatoka kwa mtu
unayemfahamu, mpigie aliyekutumia ujumbe kwa namba nyingine ili
kuthibitisha’’ alifafanua Semu.
Alitahadharisha kuwa mtu akipokea
taarifa kwa njia ya simu au ujumbe mfupi wa maandishi kuwa ametumiwa
fedha kimakosa na kutakiwa kuzirudisha asifanye hivyo mpaka
atakapojiridhisha na uhalali wa taarifa hiyo.
Akizungumzia matumizi ya huduma za
kifedha kwa njia ya mitandao, Semu alibainisha kuwa kwa miezi miwili ya
Novemba na Desemba 2016 jumla ya fedha iliyopita kwenye mitandao ya
simu za mkononi ni shilingi trilioni 13.07 hali inayothibitisha ongezeko
kubwa la matumizi ya huduma za kifedha kwa njia ya mitandao hapa
nchini.
Alitaja makampuni yaliyohusika na
takwimu za miamala hiyo kuwa ni Zantel (EASY PESA), Tigo (TigoPesa),
Vodacom (M PESA), Airtel (Airtel Money) na Halotel (HALOPESA).
Aidha aliwataka wananchi kutoa
taarifa polisi kuhusu matapeli na kuwasilisha malalamiko yao ya huduma
za mawasiliano kwa TCRA kupitia sanduku la posta 474 Dar es salaam au
wafike kwenye ofisi za TCRA zilizo karibu au wapige simu namba 0784
558270, 0784 558271 na barua pepe (malalamiko@tcra.go.tz)
0 comments :
Post a Comment