Jenerali Ulimwengu Aiomba Mahakama Imuunganishe Katika Kesi ya Mbowe Dhidi ya Makonda


Mwanahabari nguli Jenerali Ulimwengu, leo anatarajia  kuwasilisha maombi Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, akiomba kuungana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe  katika kesi ya katiba iliyofunguliwa hivi karibuni.

Ulimwengu anaomba kuunganishwa katika kesi ya katiba namba 1 ya 2017 kama mdai dhidi ya wadaiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam na Ofisa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

“Maombi ya kumuunganisha yameandaliwa na kesho(leo) yatakuwa mahakamani kuomba naye awe mdai. Anaomba kujiunga kwa kuwa mambo anayopigania Mbowe naye ana maslahi nayo kwa sababu ni mambo muhimu ya katiba,” alisema mmoja wa jopo la Mawakili kutoka Kurugenzi ya Katiba Sheria na Haki za Binadamu ya Chadema, Peter Kibatala.

Katika kesi hiyo ya katiba, Mbowe anaomba Mahakama Kuu itamke   kuwa Mkuu wa Mkoa hana mamlaka ya kudhalilisha na kukamata.
 
Mbowe pia anaomba mahakama itengue vifungu vya 5 &7 vya Sheria ya Tawala za Mitaa kwa kuwa ni batili na vinakiuka haki ya katiba.

Mbowe alifungua kesi hiyo akidai Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amekiuka sheria na taratibu katika kushughulikia watuhumiwa wa biashara ya dawa za kulevya nchini.

Kesi hiyo ya katiba inasikilizwa na majaji watatu, Jaji Sakieti Kihiyo, Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Khaday.

Baada ya kufungua kesi hiyo Mbowe pia aliomba mahakama itoe amri asikamatwe mpaka maombi yake ya zuio yatakaposikilizwa na kutolewa uamuzi.

Mahakama ilitoa zuio la muda kwa Jeshi la Polisi  kutomkamata Mbowe hadi maombi yake ya kupinga kukamatwa aliyowasilisha mahakamani yatakaposikilizwa.

Maombi hayo yalitakiwa kusikilizwa mwishoni mwa wiki lakini upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Gabriel Malata uliwasilisha pingamizi, ukiomba mahakama iyatupilie mbali kwa sababu  hana msingi katika sheria.

Upande wa mdai ulijibu hoja za kupinga maombi yao na Mahakama ilisikiliza hoja za pande zote mbili na kupanga kutoa uamuzi wa pingamizi hilo Machi 2, mwaka huu.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment