Wakati hoja za kisheria zilizotolewa na Wakili Tundu Lissu anayemtetea
mdaiwa katika rufaa ya kupinga matokeo ya ushindi wa Mbunge wa Bunda
Mjini, Ester Bulaya zilikwamisha usikilizwaji wa shauri hilo, Dk
Masumbuko Lamwai anayemwakilisha aliyekuwa mgombea wa CCM Jimbo la
Longido, Steven Kiruswa, ameomba mahakama kuitupilia mbali rufaa ya
Onesmo ole Nangoro wa Chadema.
Akiwasilisha ombi lake, Wakili Lissu alidai waleta rufaa walikiuka
kifungu cha 106(viii) cha sheria kinachoelekeza mjibu rufani kupewa
nakala za hoja za rufaa, angalau siku 30 kabla ya shauri kusikilizwa.
Aliieleza Mahakama kuwa alipokea hoja hizo kwa barua pepe Februari 11.
Wakili wa wadai, Costantine Mutalemwa alikiri kuwasilisha hoja hizo kwa
njia hiyo baada ya kuwasiliana kwa simu na wakili mwenzake, madai ambayo
Lissu aliyakana akisisitiza kuwa msomi mwenzake huyo alipaswa
kuwasilisha hoja ofisini kwake jijini Dar es Salaam ndani ya muda
unaokubalika kisheria.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufaa; Augustine Mwarija, Shaaban
Lila na Salim Mbarouk liliahirisha shauri hilo namba 199/2016, baada ya
kukubaliana na maombi ya Wakili Lissu ya kupewa muda wa kutosha kupitia
hoja za warufani.
“Kwa kuzingatia maombi ya wakili wa mjibu rufaa, Mahakama imeona ni
vyema shauri hili liahirishwe hadi siku nyingine kumpa muda wa kutosha
kujibu hoja kama kanuni zinavyoelekeza,” alisema Jaji Lila.
Jaji Lila alisema pande husika zitajulishwa na Ofisi ya Msajili tarehe ya shauri hilo kusikilizwa.
Novemba 17 mwaka jana, Jaji Noel Chocha wa Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza
alimtangaza Bulaya kuwa mshindi halali baada ya kutupilia mbali maombi
ya wapiga kura wanne; Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na
Acetic Malagila waliofungua kesi kuomba ushindi huo utenguliwe.
Katika tukio jingine, Dk Lamwai ameomba majaji wa rufaa kutupilia mbali
rufaa ya kupinga kufutwa kwa matokeo yaliyompa ushindi aliyekuwa
Mbunge wa Longido, Onesmo ole Nangole (Chadema).
Akiwasilisha pingamizi hizo jana mbele ya majaji; Bernard Luanda, Musa
Kapenka na Stella Mugasha, Dk Lamwai alidai kuwa notisi ya kukata rufaa
iliyowasilishwa na mrufani haikuzingatia masharti ya kisheria
aliyoangizwa na mahakama.
Alidai kuwa Novemba mwaka jana, mahakama ilitoa maelekezo ya kufanya
marekebisho kwenye notisi ya rufaa ikiwamo kumjumuisha mshtakiwa wa pili
na wa tatu na kwamba, licha kurekebisha hayo kwenye notisi hiyo
walikiuka kifungu cha kanuni za Mahakama ya Rufaa 96 (i)(a-k), mbavyo
licha ya kuwekwa kwa washtakiwa hao havikutaka uamuzi wa mahakama
kuwekwa kwenye notisi hiyo.
Wakili wa mrufani, Method Kimomogoro alikiri kuongeza kurasa kwenye
rekodi hiyo lakini haziathiri mwenendo wa kesi kwani, zinahusu
marekebisho yaliyoagizwa na mahakama ya kuongeza washtakiwa na uamuzi wa
korti.
Baada ya kutolewa hoja hizo, Jaji Luanda alitaka mahakama kupewa muda
ili kutafakari mapingamizi hayo na kuamua iwapo rufaa hiyo iendelee, au
ifutwe.



0 comments :
Post a Comment