Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu ametaja kasoro kadhaa katika
zoezi la vita ya dawa za kulevya lililoanzishwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar
es salaam Paul Makonda.
Amesema, Kwanza, Mkuu wa Mkoa hana mamlaka yoyote ya kuelekeza
watu kwenda kuripoti polisi. Hii ni licha ya mamlaka yake kama
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na mamlaka yake ya
kipolisi yapo chini ya Sheria ya Tawala za Mikoa.
Pili, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Jinai, kila mtu ana
wajibu wa kutoa taarifa ya kosa la jinai analoona limetendeka kwa
polisi. Hii ni ile inayoitwa kufungua RB. Mkuu wa Mkoa Makonda alitakiwa
afungue RB kwa wote anaowatuhumu kufanya biashara ya madawa. Hajafanya
hivyo na ni kosa la jinai kutokufanya hivyo.
Tatu, kwa kutumia mamlaka yake ya kipolisi, Mkuu wa Mkoa Makonda
alikuwa na uwezo wa kuamuru wale wote anaowatuhumu kufanya biashara ya
madawa kukamatwa na kuwekwa kizuizini kwa masaa 48 na baadae kufikishwa
mahakamani. Badala ya kuamuru 'wahalifu' hawa wakamatwe, Mkuu wa Mkoa
Makonda aliwaelekeza wajipeleke polisi kwa mahojiano.
Nne, kwa kuzingatia hatari kubwa ya madawa ya kulevya kwa jamii
yetu, sheria husika za nchi zimeweka adhabu ya chini kabisa ya kifungo
cha miaka 20 kwa wanaothibitika na mahakama kuhusika na biashara hiyo.
Aidha, makosa ya madawa ya kulevya hayana dhamana kisheria. Iweje wale
wote waliotuhumiwa na Mkuu wa Mkoa Makonda wamepelekwa mahakamani lakini
wote wamepewa onyo tu au wamepewa dhamana Mahakamani.
Kati ya mapolisi 11 waliotuhumiwa, hakuna hata mmoja aliyepelekwa
mahakamani na kushtakiwa kwa tuhuma hizi. Badala yake, tunaambiwa
wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa polisi dhidi yao. Kwa mujibu wa
Sheria zetu za ajira, mtumishi anayesimamishwa kazi analipwa mshahara
kamili kwa muda aliosimamishwa
Tano, kitendo cha kuwatangaza watuhumiwa kwa namna alivyofanya
Mkuu wa Mkoa Makonda, kesi yoyote itakayofunguliwa dhidi yao
itaharibika. Kila mtuhumiwa atajitetea kwamba amekamatwa na kushtakiwa
kwa sababu za kisiasa na kwa amri haramu za Mkuu wa Mkoa. Kila mtuhumiwa
atajitetea kwamba hakuna RB yoyote iliyofunguliwa dhidi yake na kila
wakili wa utetezi atataka Mkuu wa Mkoa Makonda aitwe mahakamani kwa
ajili ya kuhojiwa. Makonda ataliwa nyama na mawakili kwenye
cross-examination. Kwa kifupi, hii sio vita dhidi ya wauza 'unga', hii
ni political charade na character assassination inayofanywa kwa mbinu za
ovyo kabisa bila kufuata sheria Haitafika popote.
0 comments :
Post a Comment