Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amewapongeza Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa juhudi kubwa
walizofanya kunusuru maisha ya Neema Mwita Wambura ambaye alijeruhiwa
kwa kuunguzwa na maji ya moto kifuani, shingoni na mkononi.
Pongezi
hizo za Mhe. Dkt. Magufuli zimetolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya
Rais, Ikulu Bw. Gerson Msigwa muda mfupi baada ya kumfikisha Neema Mwita
Waitara katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambako Rais Magufuli
ameagiza apelekwe kwa mara nyingine kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa
maendeleo ya afya yake.
Katika
Pongezi hizo Mhe. Dkt. Magufuli amesema Madaktari wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili wamefanya kazi kubwa na ya kizalendo kuhakikisha Neema
anapona licha ya majeraha makubwa aliyoyapata miaka miwili iliyopita na
ambayo yalitishia uhai wake.
Pia
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mama Mariam Amir (Bibi Mwanja) kwa
upendo wake wa kumchukua Neema na kisha kumpa hifadhi nyumbani kwake
huko Tandika Devis Kona Jijini Dar es Salaam.
“Nakushukuru
sana Mama na ninakupongeza, umeonesha mfano mzuri wa kujali umoja na
upendo kwa Watanzania wenzako bila kujali dini, kabila wale kanda
unayotoka na hivi ndivyo Watanzania wote tunapaswa kufanya” amesema Mhe.
Rais Magufuli.
Kabla
ya kutoa pongezi hizo, mapema leo asubuhi Mhe. Rais Magufuli amewatuma
wasaidizi wake wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu
Bw. Gerson Msigwa kwenda Tandika Devis Kona katika Wilaya ya Temeke
Jijini Dar es Salaam kumuona Neema Mwita Wambura ambaye alipatiwa
hifadhi katika nyumba ya Mama Mjane aitwaye Mariam Amir (Bibi Mwanja)
baada ya kuona picha na kusoma taarifa za mkasa uliomkuta katika
mitandao ya kijamii.
Mhe.
Rais Magufuli ametoa Shilingi laki 5 kwa Neema kwa ajili ya kumsaidia
chakula yeye na watoto wake waliohifadhiwa na rafiki yake huko Bunda
Mkoani Mara na pia ametoa Shilingi laki 5 kwa Mariam Amir aliyejitolea
kumsaidia na kumpa hifadhi nyumbani kwake. Pia ameahidi kumsaidia wakati
wote wa matibabu na pia familia yake.
Baada
ya kumpokea daktari bingwa wa magonjwa ya dharula na ajali katika
kitengo cha dharula cha Hospitali ya Taifa Muhimbili Dkt. Juma Mfinanga
amesema wameanza kumfanyia uchunguzi ili kujua maendeleo yake na kama
kumpa matibabu zaidi.
Nae
Daktari Bingwa wa Upasuaji Dkt. Ibrahim Mkoma ambaye amekuwa akimfanyia
matibabu Neema Mwita Wambura tangu Julai 2015 alipofikishwa hospitalini
hapo kwa mara ya kwanza amesema Neema anaendelea vizuri baada ya
kufanyiwa upasuaji mara nne.
Dkt.
Mkoma amesema baada ya upasuaji huo, sasa Neema anaweza kuinua na
kugeuza shingo yake na kwamba kwa sasa wataendelea kumfanyia uchunguzi
zaidi ili kujua maendeleo yake. Mhe. Rais Magufuli ameagiza vyombo vyote
vinavyohusika kufanyia kazi mkasa uliomkuta Neema Mwita Wambura na
kuhakikisha haki inatendeka.
0 comments :
Post a Comment