WAKATI mwili wa bilionea na mfanyabiashara maarufu wa vinywaji Festo Mselia (58), ukitarajiwa kuzikwa kesho katika kijiji cha Umbwe Unana mkoani Kilimanjaro, mambo mapya yameibuka kuhusiana na kifo chake kinachodaiwa kutokana na kujipiga risasi.
Mambo mapya yaliyoibuka yakihusishwa na chanzo cha kifo hicho ni pamoja na usumbufu alioupata polisi, kutuma ujumbe wa kumuaga mkewe na kumpigia simu mdogo wake mara tisa bila kupokewa muda mfupi kabla ya umauti kumfika.
Akizungumza na Nipashe jana, mdogo wa marehemu huyo, Anthony Mselia alisema mwili wa marehemu baada ya kufanyiwa uchunguzi, umekutwa na matundu matatu ya risasi kwenye maeneo ya chini ya kidevu.
"Mazingira yanaonyeshwa kwamba 'brother' (kaka) hajauliwa na mtu, yaani sielewi ni kitu gani kilichomsibu," alisema.
"Lakini kulikuwa na taharuki kuhusu suala la pombe kali aina za viroba, lakini hakuna kitu alichowahi kuniambia zaidi ya kulalamikia suala hilo.
"Tangu siku ya kwanza alipokamatwa Machi 3, mwaka huu, alinipigia simu na kuniambia kwamba serikali haioni namna yeyote ya kuongeza muda na hii ilitokana na kwamba alikuwa na mzigo mkubwa wa bidhaa hiyo katika stoo zake zaidi ya tatu tofauti wenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni moja na viroba ndio vilivyokuwa na mzunguko mkubwa wa biashara na ndivyo vilikuwa vimekamata fedha."
Akisimulia zaidi, mdogo huyo wa marehemu alisema kaka yake aliwapeleka polisi zaidi ya stoo tatu.
Alisema kuwa kabla kaka yake hajafikia uamuzi huo Machi 7, yeye alifika nyumbani kwake na kumuaga kuwa anasafiri kwenda Moshi.
"Nilimsalimia na kumuaga kwa safari na akaniruhusu kuondoka na hakuonekana kuwa na mawazo wala kitu chochote alikuwa 'happy' (na furaha) tu. Nakumbuka aliniambia kwamba mdogo wangu ukienda uwahi kurudi kutoka Moshi kwa kuwa mimi naishi hapa hapa Dodoma," alisema.
Aliendelea kueleza kuwa anaamini kaka yake hajafikia uamuzi huo kutokana na kuwa na madeni aliyokuwa nayo ambayo alidai alikuwa ameshayalipa kwa kiasi kikubwa.
"Kwa mfanyabiashara mkubwa kama Mselia ambaye ana mzunguko mkubwa wa biashara, lazima kutakuwa na watu wanaoleta mizigo lakini siyo kesi ya yeye kufikia hatua hiyo, mimi mpaka sasa hivi akili na aliponipigia simu na kulalamika kilichompelekea kufanya uamuzi ni suala la viroba."
Alieleza kuwa awali polisi, maofisa wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) walifika dukani kwa kaka yake kumhoji na kumkagua na kwamba marehemu alitoa ushirikiano na kuwapeleka kwenye stoo zake na kuwaonyesha mzigo wote ambao alizuiwa kuuuza.
Alisema kuwa maofisa hao baada ya kumaliza kukagua, waliweka stika lakini alikuwa bado analalamika kwanini mzigo wenye thamani kubwa ya fedha ufungiwe ndani, jambo ambalo lilikuwa linampa wakati mgumu.
Alisema mzigo huo licha ya kuzuiwa kuuzwa, bado umo kwenye stoo zake.
SIMU MARA TISA
Mdogo huyo wa marehemu aliendelea kusimulia kuwa baada ya kuagana na kaka yake, hakuwasiliana naye lakini baada ya kufika Moshi na kutaka kumjulisha kwamba amefika salama, alibaini kuwa kaka yake alikuwa amempigia simu mara tisa bila kumpokea.
"Muda mfupi baadaye nilipigiwa simu na polisi kwa namba zilizoishia 71 akiuliza kwamba 'wewe unamfahamu Mselia?',
nikamwambia ni kaka yangu, akaniambia mimi ni askari, kaka yako amejipiga risasi, nikamuuliza amejipiga au imemfyatukia bahati mbaya?
"Akasema amejipiga mwenyewe, tafuta watu waende ‘General Hospital’ (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa) kwa ajili ya kumpa msaada."
Alibainisha kuwa baada ya taarifa hiyo, alimpigia mke wa marehemu na baadaye wakawapigia marafiki wa karibu wa familia na wakaungana naye, lakini muda mfupi baadaye akapigiwa simu kuwa kaka yake amefariki.
Alidai kuwa marehemu alikuwa anamshirikisha matatizo yote ya kibiashara.
KWAHERI
Mdogo huyo wa marehemu pia alidai kuwa kaka yake alitumia ujumbe mfupi wa maandishi kwa mkewe uliosomeka "kwaheri" muda mfupi kabla ya tukio la risasi, lakini mke wake hakuutilia maanani akidhani alikosea kuutuma kwake badala yake alikuwa anamuaga mtu mwingine.
"Lakini baadaye, baada ya kupata taarifa kuwa amejipiga risasi, aligundua kuwa kumbe alikuwa anamuaga," alisema Mselia.
"Kinachoonekana ni 'harrasment' ya polisi kwa sababu polisi walifika mara ya kwanza, ya pili na ya tatu, Mselia wa watu maskini hapendi kusumbuliwa."
KAULI YA POLISI
Akizungumza na Nipashe kwa simu jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, alidai maganda ya risasi yaliyokutwa pembeni ya mwa mwili wa marehemu yalitumiwa na marehemu wakati akijaribu kujiua.
“Maganda yale ya risasi aliyatumia kujipiga mwenyewe, unajua alipokuwa akijipiga nadhani hakujilenga vizuri na hii ni kutokana na kupaniki, alijipiga kwenye shigo ikatokea mdomoni, hakufa na yeye alitaka afe sasa kutokana na kujipiga kule alijipiga risasi tano," alidai Kamanda Mambosasa.
Mfanyabiashara huyo alijiua juzi shambani kwake Msalato Manispaa ya Dodoma baada ya kuhojiwa na polisi kuhusu shehena ya viroba aliyokuwa nayo yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni moja.
0 comments :
Post a Comment