Mashabiki Wa Yanga Wamlaumu Kocha


Dar es Salaam. Yanga imesononesha mashabiki wake huku ikijiweka katika mazingira magumu ya kufuzu kwa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Zanaco ya Zambia.

Ugumu wa matokeo hayo ni kwamba, Zanaco watataka kushinda ama kutoka suluhu huku salama ya Yanga ni sare ya 2-2 au ushindi.

Hata hivyo, timu itakayopoteza mchezo wa marudiano, itashuka hadi michuano ya Kombe la Shirikisho. Timu hizo zinarudiana kati ya Machi 17 na 19 mjini Lusaka, Zambia.

Mabadiliko Yanga

Bao la Simon Msuva la dakika ya 37 liliwafanya Yanga kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa uongozi wa bao 1-0.

Kipindi cha pili kilikuwa bora zaidi kwa Zanaco walioonekana kutaka kurudisha bao na kufanya mashambulizi mengi bila umakini.

Mghana, Attram Kwame alisawazisha bao hilo kwa Zanaco dakika ya 79 na kufanya mchezo huo kuwa mgumu zaidi kwa wenyeji.

Sare hiyo imezua maswali kwa kocha wa Yanga, George Lwandamina, ambaye ameshindwa kuonyesha cheche zilizoonekana msimu uliopita ndani ya kikosi hicho kwa mujibu wa mashabiki wa klabu hiyo.

Mashabiki wa Yanga walishindwa kuamini kilichotokea baada ya filimbi ya mwisho, wakiishuhudia timu yao ikikosa mabao ya wazi na wakati mwingine kupoteana hasa kipindi cha pili.

Kilichozua maswali mengi hasa ni baada ya Lwandamina kufanya mabadiliko ya kumtoa Donald Ngoma na Thabani Kamusoko na nafasi zao kuchukuliwa na Emmanuel Martin na Juma Mahadhi.

Inawezekana ni kutokana na wachezaji hao kuwa majeruhi wa muda mrefu.

Hata hivyo, mabadiliko hayo hayakuwa na msaada kwa Yanga kwani kiungo kilipwaya na mipira ikawa haitulii mbele.

Hali hiyo iliisaidia Zanaco na kutawala sehemu ya kiungo huku ikipandisha mashambulizi mfululizo na kuipa kazi safu ya ulinzi ya Yanga kuondosha mipira ya hatari.

Mabeki Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Vincent Bossou, Hassan Kessy na Haji Mwinyi walikuwa na wakati mgumu muda wote wa kipindi cha pili.

Mchezo ulivyokuwa:

Yanga ilianza kwa kasi na kutunmia vizuri uenyeji wao wakionekana kujiamini huku kikosi chao kikiwa na mabadiliko kadhaa katika upangaji.

Mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Ngoma alianza kwa mara ya kwanza tangu alipocheza kwa mara ya mwisho mwaka jana ndani ya kikosi hicho.

Kiungo mkabaji, Kamusoko alichezeshwa kama mshambuliaji wa pili akisaidiana na Ngoma, wakati Obrey Chirwa alitokea kushoto na kulia akisimama Msuva.

Zanaco wangeweza kuandika bao la kuongoza mapema katika mchezo huo kupitia kwa Ernest Mbewe, lakini uimara wa kipa Deo Munishi ‘Dida’ ulimnyima nafasi ya kufunga.

Yanga walibadili upepo na dakika ya 10 wangeweza kupata bao la kuongoza, lakini Ngoma na Msuva walijikuta wakiwania mpira mmoja na kuukosea wakiwa ndani ya eneo la hatari.

Ngoma, ambaye alikuwa mwathirika wa faulo kila wakati kipindi cha kwanza alifanikiwa kupiga pasi safi kwa kiungo Justine Zulu, ambaye nae alifinya mpira ndani uliomkuta Msuva.

Akiwa katika mwendo, Msuva alikutana na pasi fupi ya Zulu na kuingia katikati ya mabeki wawili wa Zanaco kabla ya kumchambua kipa, Racha Kola.

Bao hilo liliwapa Yanga matumaini ya ushindi katika mchezo huo kabla ya mambo kubadilika kipindi cha pili.

Kasi ya Zanaco ya kipindi cha pili iliwafanya Yanga kuchoka na kuonekana kuzidiwa katika kiungo.

Saith Sankala aliyekuwa akiisumbua safu ya ulinzi ya Yanga alifanikiwa kukunja vizuri krosi iliyotua nguzo ya pili ya lango na kuunganishwa vizuri na Kwame kuandika bao la kusawazisha.

Bao hilo ni faida kubwa kwa Zanaco, ambao wanaweza kufuzu kwa hatua ya makundi hata kwa sare ya bila kufungana katika mchezo wa marudiano nchini Zambia wiki ijayo.

Simba washangilia

Mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Simba walilipuka kwa furaha baada ya Kwame kufunga bao la kusawazisha kwa Zanaco.

Mashabiki hao, ambao walikuwa eneo maarufu linalotumiwa na wadau wa Simba, walikuwa kimya kwa muda mrefu kabla ya Kwame kuwainua dakika ya 79.

Awali, walianza kushangilia kila shambulizi la Zanaco linapotokea kabla ya kuamua kunyamaza dakika ya 37 kutokana na bao la Msuva.

Hadi kumalizika kwa mchezo huo, mashabiki hao walionekana kuridhishwa na matokeo na kuungana na mashabiki wachache wa Zanaco kushangilia.

Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi alisema: “Tumeyapokea matokeo, tunajipanga kwa marudiano.Tumefungwa bao kwa vile mabeki hawakuwa makini, lakini pia wachezaji walikuwa na uchovu baada ya kucheza mechi mfululizo.”

Naye kocha wa Zanaco, Mumba Mumamba alisema wamefurahia sare hiyo na wanajipanga kwa mchezo wa marudiano wakiamini watafanya vizuri.

Kikosi cha Yanga: Dida, Kessy, Mwinyi, Nadir, Bossou, Yondani, Msuva, Zulu, Kamusoko/Mahadhi, Ngoma/Martin na Chirwa.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment