Waziri
wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema atajiuzulu
uwaziri endapo mtu atampelekea ushahidi wa kuwa na uhusiano wa
kimapenzi na msanii yeyote.
Kauli
hiyo ya Nape inakuja ikiwa ni takriban wiki tatu tangu Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda, aseme watu wanaotetea wale aliowataja
hadharani kwa kuhusika na dawa za kulevya wengine ni wapenzi wao.
“Wengine wanaumia tunagusa wapenzi wao, wawasaidie waache si kupiga kelele tu, ujumbe umefika,” alisema Makonda katika moja ya mikutano yake.
Ingawa
katika mkutano huo Makonda hakumtaja mtu kwa jina, lakini aliitoa kauli
hiyo siku chache baada ya Nape kupinga mfumo wake wa kutaja majina ya
watu hadharani, hususani wasanii na kuwatuhumu kuhusika na dawa za
kulevya.
Nape alisema kuwataja watu bila ushahidi ni kuwachafulia majina yao waliyoyatengeza kwa muda mrefu.
Mbali
na Nape, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM), alizungumza
mara kadhaa bungeni akimpinga Makonda kwa mfumo wake aliokuwa akitumia,
kutaja majina ya watu wanaojihusisha na dawa za kulevya.
Akizungumza
katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha luninga cha ITV
juzi, Nape alieleza kushangazwa na kitendo cha kuhusishwa kuwa na
mahusiano na wasanii.
“Ila
kama mtu ana ushahidi alete hapa mezani aseme Nape hili unalofanya,
unafanya kwa sababu una uhusiano, na mtu akileta najiuzulu uwaziri.
“Hii
ni katika watu ambao wanakosa hoja halafu wanasingizia hoja ambazo
hazina msingi, ningefurahi mtu akisema Nape hana sababu ya kutumia
busara, twende na hoja hii nyingine ni upuuzi,” alisema Nape.
Akizungumzia
kuhusu kutajwa kuhusishwa kuwa na mahusiano ya kimapenzi na msanii
nyota wa filamu, Wema Sepetu, Nape alisema wasanii wengi ni wadogo zake
akiwamo Wema.
“‘Majority’
ya wasanii hawa ni wadogo zangu. Wamezungumza habari ya Wema, sasa
nieleze ukweli kwamba baba yake, mzee Sepetu (Isack) na baba yangu
(Moses Nnauye) ni mtu na kaka yake, kwa hiyo Wema ni mdogo wangu sana
sana.
“Mama
yake anatoka Singida, mama yangu naye anatoka Singida, ni mtoto mdogo
lakini mtu akiamua apoteze ‘direction’ (mwelekeo) ya mjadala anaweza
kuja na hoja nyingi sana.
“Mimi
nimeanza kufanya kazi na wasanii, nimefanya nao kazi kwa miaka 16, hii
ya uwaziri imekuja juzi tu. Pia msisahau hawa wasanii tuliwatumia kwenye
kampemi ya CCM, mimi ndiyo nilikuwa Katibu wa Uenezi wa CCM.
“Ukizungumza
burudani, hamasa na ‘publicity’ mimi ndio nashughulika nayo, hivyo
kuwaingiza wasanii kwenye kampeni haikuwa kazi rahisi, sasa nikiwa nao
karibu dhambi inatoka wapi, maana ndio nilipewa dhamana ya kuwasaidia.
Hizi hoja zingine ni za kijinga kabisa,” alisema Nape.
Pamoja
na mambo mengine, Nape alisema utaratibu uliokuwa ukitumiwa na Makonda
kwa kutaja majina ya watu hadharani una madhara makubwa kwani unajenga
chuki katika jamii.
Nape
ambaye pia ni mbunge wa Mtama mkoani Lindi, alisema hakuna mahali
popote duniani vita ya dawa za kulevya ilishinda kwa kupiganwa
hadharani.
“Tutajenga
chuki kubwa sana kwenye jamii kama tukianzisha utaratibu wa kila mtu
anasimama anamtaja mtu hadharani, ukishamtaja anaandikwa kwenye
mitandao.
“Nchi
itaingia kwenye vurugu kubwa bila sababu na wale wenye chuki zao
watapitia hapo kuanza kutajana majina, tukitajana majina hadharani, hii
vita hakuna mahali walipigana hadharani wakashinda popote duniani,
haipo,” alisema.
Aidha alisema watu wasihukumiwe bila kosa bali haki itendeke na sheria na taratibu zifuatwe.
“Namshukuru
Rais (Dk. Magufuli) ametumia busara namna ya kuli-handle
(kulishughulikia) hili suala, amemteua kamishna na amemkumbusha waziri
mkuu kwamba yeye ndie mwenyekiti wa hii kamati na mawaziri wako ndio
wajumbe, sasa ameweka vita hii katika chombo salama.
“Pia
namshukuru kamishna mwenyewe kasema tusitaje majina hadharani, lakini
tufuate sheria na akasema hakuna jiwe litabaki juu ya jiwe,
tutahakikisha tunasimamia sheria,” alisema Nape.
0 comments :
Post a Comment