Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (MB) akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kutoa tamko juu ya hatua walizochukua za kupambana na ugonjwa wa Ebola
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Ummy Mwalimu (MB) mapema leo Mei 29.2017, amekutana na vyombo vya habari na kuzungumzia juu ya Ugonjwa wa Ebola ambao umelipotiwa kutokea nchi jirani ya DRC Congo, ambapo amewatoa hofu wananachi wa Tanzania huku akiwahakikishia usalama wa afya zao kwani tayari vifaa, mafunzo na elimu juu ya kujikinga na Ebola Wizara yake inasimamia ipasavyo.
Waziri Ummy Mwalimu amebainisha kuwa, awali alikuwa katika mkutano mkuu wa Afya wa Dunia ambapo moja ya ajenda katika mkutano huo ni suala la ugonjwa wa Ebola ambao hadi sasa katika nchi hiyo ya DRC Congo ina wagonjwa waliothibitika na kufikia 43.
“Kama tulivyowatangazia kwenye taarifa yetu ya Tarehe Mei 15 mwaka huu. Wizara yetu ilipata taarifa kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa Ebola katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) uliotangazwa na Shirika la Afya Duniani siku ya tarehe 12 Mei, 2017. Ugonjwa wa Ebola umethibitishwa kwa kupitia vipimo vya maabara na hadi tarehe 21 Mei, 2017.
Dkt. Azma Simba (mwenye kitambaa chyeusi kichwani) ambaye ni mtaalam wa kufuatilia magonjwa ya Milipuko akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa Habari wakati wa tuko la Waziri Ummy akitoa tamko la namna Tanzania inavyopambana na Ebola.
Idadi ya Wagonjwa imeendelea kuongezeka na kufikia 43 ambapo kati ya hao wagonjwa 4 walipoteza maisha na wengine wanaendelea kupata matibabu katika vituo mbali mbali vya kutolea huduma za afya nchini humo. Ugonjwa huu umetokea katika Jimbo la North-east Bas-Uele linalopakana na nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) kukiwa na taarifa za kuenea katika maeneo mengine matano ya jirani yakiwemo Nambwa, Muma, Ngayi, Azande na Ngabatala.
Wengi wao wamekuwa na dalili za Homa, Kutapika na Kuharisha Damu pia kutokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili.” Alieleza Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy ameeleza kuwa, kwa hatua walizochukua kwa sasa hapa nchini licha ya kutokuwa na mgonjwa yoyote aliyehisiwa au kuthibitishwa kuwa na virusi vya Ebola hadi wakati huu, wameamua kutoa elimu na kuchunguza kwa makini watu wote wanaoingia katika mipaka yote ya Tanzania hasa wale wanaotoka nchi za Congo.
“Wizara imetoa tahadhari ya ugonjwa huu kwa wananchi katika Mikoa yote na hasa ile inayopakana na nchi jirani na DRC Congo.Mikoa hiyo ni pamoja na Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya na Songwe.
Tayari viongozi wote wamepatiwa elimu na namna ya kujikinga kuanzia ngazi ya chini mpaka juu wakiwemo Makatibu Tawala na Waganga Wakuu wote wa Mikoa kupitia Wizara ya TAMISEMI na mamlaka zingine zote kutoa tahadhari ya ugonjwa huu na kuweka mikakati thabiti ya udhibiti magonjwa” alieleza Waziri Ummy.
Na kuongeza kuwa, timu za Wataalamu kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na TAMISEMI zipo mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Mwanza, Kagera, Kigoma, Katavi, Rukwa, Mbeya na Songwe wakiendelea na mikakati ya namna ya kudhibiti ugonjwa huo hii pia ni pamoja na kuingia mipakani katika kudhibiti wasafiri watokao Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Waziri Ummy Mwalimu pia amesema wameanzisha mfuo wa ufuatiliaji wa magonjwa “Integrated Disease Surveillance and Response” mafunzo ambayo yanatolewa katika mikoa yote inayopakana na nchi jirani ya Jamhuri ya Kongo.
Aidha, Waziri Ummy amesema vifaa walivyotoa katika kupambana na ugonjwa huo hasa katika mikoa jirani na Congo, ni pamojana Gauni la kujikinga, miwani (google), na Buti (Boots), Pia ugawaji wa vidonge vya klorini kwa ajili ya kuzuia maambukizi kwa wafanyakazi wa afya (Infection, Prevention and Control measures) huku ikipeleka seti 100 za vifaa kinga vya kuzuia maambukizi ya ugonjwa wa Ebola katika kila MSD zones ( Mwanza, Tabora, Moshi, Mbeya).
Miongoni mwa hatua zaidi ni pamoja na kuhakikisha wanapima raia wote wanaotokea nchi za Congo kwa hatua za haraka, Hii ni pamoja na ukaguzi ikiwemo upimaji wa joto la mwili (Thermal Screening) kwa wasafiri wanaotoka au kupitia Jamhuri ya Kongo. Ambapo wameagiza mashine 4 za nyongeza kwa ajili ya “Thermal Screening” kwa mipaka yote ikiwemo ya Horohoro,Mutukula, Rusumo na Sirari ili kuimarisha ufuatiliaji huu.
Waziri Ummy amesema hadi sasa kuna jumla ya Thermal Scanner 11 na baadhi zipo kwenye matengenezo katika Point of Entries (Songwe Airport, Tunduma, Namanga, Tarakea, Kabanga, Murongo, Kigoma sea port, Kigoma Airport, Manyovu, Mabamba, Mwanza Airport na JNIA).
“Kuanzisha rejesta ya kurekodi wasafiri ambao watakuwa wametoka katika Jamhuri ya Kongo ili kuweza kuwafuatilia kwa karibu iwapo watapata dalili za ugonjwa huu. Aidha Pamoja na rejesta, wasafiri watakaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo watapaswa kujaza fomu maalamu ili kuweza kupata taarifa zao na ili kurahisisha ufuatiliaji wa wasafiri hawa iwapo wataonesha dalili za ugonjwa huu” Ameeleza Waziri Ummy Mwalimu.
Waziri Ummy amemalizia kwa kusema kuwa, Wizara inaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na Shirika la Afya Duniani (WHO), US-CDC pamoja na mashirika mengine ya Kimataifa kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Kimataifa na Kitaifa. Kwa sasa Wizara inapokea taarifa ya kila siku ya Ugonjwa wa Ebola, na kuzifanyia tathmini kwa karibu na kutoa maelekezo kwa Maofisa Mbalimbali wakiwemo Waganga wakuu wa Mikoa ili kuona jinsi hali inavyoendelea na kuboresha mipango yote ya Taifa katika kuwalinda wananchi wake.Facebook