IGP Sirro akaribishwa kwa mauaji Kibiti

Kibiti. Watu wasiojulikana juzi usiku waliua mkazi mwingine wa Ikwiriri, ikiwa ni saa chache kabla ya mkuu mpya wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro kutekeleza ahadi yake ya kukutana na wazee wa wilaya hizo za mkoani Pwani kuzungumzia visa hivyo.
Wilaya za mkoani Pwani za Rufiji, Kibiti na Mkuranga zimekuwa zikikumbwa na mauaji dhidi ya viongozi wa vijiji na vitongoji tangu Mei mwaka jana na aliyeuawa juzi anakuwa mtu wa 32 kwa taarifa ambazo Mwananchi imekuwa ikizirekodi tangu mwaka jana.
Mauaji mengi yamekuwa yakifanyika usiku kwenye nyumba za viongozi hao na watu wengine ambao wamewahi kushika uongozi, Idara ya Maliasili na askari wa Jeshi la Polisi. Kati ya watu hao, ni watatu tu ndio waliouawa na polisi baada ya kukataa amri ya kusimama.
Kamanda Sirro, ambaye aliapishwa wiki iliyopita kushika nafasi hiyo, aliitikia wito wa wazee wa wilaya hizo kutaka akutane nao na jana alikuwa anaanza mazungumzo hayo, lakini akakaribishwa na taarifa za kuuawa kwa askari wa mgambo aliyepigwa risasi nyumbani kwake.
Askari huyo, Erick Mwarabu alipigwa risasi tatu na watu wasiofahamika akiwa nyumbani kwake, kitongoji cha Kazamoyo, Rufiji. Mwarabu alivyouawa Watu wa karibu na eneo hilo wamesema Mwarabu alipigwa risasi tatu na wauaji ambao walimtafuta na kumkuta akiwa amejificha uvunguni mwa kitanda chake. Iddy Malinda, mganga mkuu wa kituo cha Afya cha Ikwiriri, alisema amebaini majeraha matatu katika maeneo tofauti ya mwili wake.
“Mawili yalikuwa mbavuni upande wa kulia na moja kichwani,” alisema. Alisema katika jeraha la kichwani, Mwarabu alipigwa risasi upande wa kushoto wa shingo yake iliyoharibu kichwa. Alisema tayari mwili umekabidhiwa kwa ndugu zake kwa ajili ya mazishi.
Mkazi wa eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Simon alisema watu hao walivunja mlango wa nyumba ya Mwarabu saa 9:00 usiku kisha kuingia ndani na kufanya mauaji hayo. Simon alisema baada ya kuingia ndani, watu hao walipitiliza hadi chumbani kwake ambako walimkuta mke wake na kumshinikiza aeleze alipo Mwarabu.
“Walimpiga sana mke wake ili awaambie alipo mume wake, lakini hakuwaeleza wauaji alipo mume wake,” alisema.
Alisema baada ya kuona hataji alipo mumewe, walimtafuta ndani ya nyumba yake na kufanikiwa kumkuta uvunguni mwa kitanda chake na ndipo walipompiga risasi akiwa uvunguni na baadaye kutoweka bila ya kuchukua kitu chochote.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Onesmo Lyanga alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo. Tukio hilo limetokea wakati Kamanda Sirro akiwa anaanza mazungumzo na wazee kutafuta mbinu ya kuwakabili wauaji.
Juni 3, wazee wa Mkoa wa Pwani walimuomba IGP Sirro kwenda wilayani Kibiti ili azungumze nao kuhusu chanzo cha mauaji hayo ya mfululizo dhidi ya viongozi wa vijijiFacebook