Ripoti ya kocha mkuu wa Yanga SC, George Lwandamina kuhusu timu hiyo kwa msimu uliomalizika wa 2016-17 na msimu ujao wa 2017-18 inaonekana kuwa na mabadiliko makubwa kutokana na mahitaji ya msimu ujao
Lwandamina ameainisha ushiriki wa timu yake katika msimu uliopita akieleza mapungufu na mafanikio yaliyowawezesha kuibuka mabingwa wa ligi kuu pia mtazamo wa kikosi chake kwa msimu ujao wa ligi kuu na ligi zingine.
Kwa upande wa madhaifu Lwandamina amelenga katika udhaifu wa timu kimbinu na kiufundi akilenga uwezo wa wachezaji wake katika kikosi chake na jinsi gani ya kuboresha ili kuitendea haki hadhi ya timu hiyo ambao wameweza kuchukua ubingwa wa ligi kuu mara 27 nchini na kuweka rekodi ya kipekee toka kuanzishwa kwa ligi hiyo.
Maeneo aliyoyaangazia ni safu ya ulinzi , akihitaji kupunguza baadhi ya wachezaji na kuleta wenye changamoto mpya . Kuleta wachezaji wenye uwezo mzuri kuichezea timu hiyo kitaifa na kimataifa tena wenye gharama nafuu.
Tayari ameonesha nia ya kumwacha beki mkongwe wa timu hiyo Oscar Joshua na kuhitaji mbadala wake kwenye nafasi hiyo ya kushoto. Oscar mlinzi wa kushoto amedumu na klabu hiyo toka Juni 2011 lakini umri na uwezo kupungua kunamfanya mzambia huyo kumfungulia mlango.
Lwandamina hana mpango wa kuendelea na mchezaji mahiri wa klabu hiyo Donald Dombo Ngoma ambaye amekuwa akisumbuliwa na majeruhi ya mara kwa mara na misuguano ya kinidhamu na uongozi, Lwandamina amelenga kuleta vijana wenye nidhamu na uwezo mkubwa katika safu yake ya ushambuliaji ili kuijenga vyema timu hiyo katika ushambuliaji.
Mateo Antony amekuwa hana nafasi ya kudumu katika kikosi chake sambamba na wenzake Juma Mahadhi na golikipa Ali Mustafa . Hawa amelenga kuwatoa kwa mkopo na nafasi zao kujazwa na wachezaji wapya ambao wapo katika mazungumzo nao.
Licha ya viungo Haruna Niyonzima na Deusi Kaseke ambao mikataba yao inakwisha mwezi Julai , lakini ameeleza bado kuwahitaji katika kikosi chake na uongozi ushuhhulikie mikataba yao . Tayari Haruna Niyonzima anahusishwa na kujiunga na mahasimu wao Simba SC na Deusi Kaseke kutua Singida United ingawa kwa nyakati tofauti wachezaji na viongozi wa timu hizo wamekana habari hizo.
Safu ya kiungo cha chini ni sehemu ya ripoti yake akilenga kumpata mtu sahihi mwenye uwezo wa asilimia 100 kuicheza nafasi hiyo . Usajili wa dirisha dogo alimsajili Zulu Justine toka Zesco United lakini ameonesha uwezo mdogo na kukumbwa na majeruhi ya mara kwa mara.
Thabani Kamusoko licha ya mara kwa mara kutumia katika nafasi sambamba na pacha wake Haruna Niyonzima lakini bado sio kiungo mkabaji asilia kuweza kuimudu vyema nafasi hiyo hususani katika mechi za kimataifa wakikutana na wachezaji wazoefu na wenye uwezo mkubwa . Fununu za chini kwa chini zinaonesha Lwandamina anamuwinda Meshack Chaila wa Zesco United pia Rafael Daudi wa Mbeya City.
Katika hatua hizo za kukiboresha kikosi chake pia Lwandamina amelenga masuala ya nidhamu na uwajibikaji . Katika ripoti yake ametanabaisha urekebishaji wa mikataba ya wachezaji kwa kuweka msisitizo wa utumishi wenye nidhamu na ufanisi wa hali ya juu akilenga makosa waliyofanya kwa mchezaji kama Malimi Busungu ambaye licha ya kugoma kuitumikia klabu lakini alikuwa akilipwa mshahara na posho mbalimbali zilizopo katika mkataba. Kwa mtazamo huo ni dhahiri Malimi Busungu ambaye mkataba wake unakwisha mwezi julai hatapata fursa kuichezea tena timu hiyo.
Uboreshwaji wa haki na masilahi ya wachezaji kuepusha migomo ya mara kwa mara kama iliyokuwepo msimu huu ambayo kwa namna moja ama nyingine ilileta athari katika harakati za ushiriki wa klabu hiyo katika ligi mbalimbali.
Idara ya tiba na matibabu hakuiacha nyuma kocha huyo. Ametoa maoni na mapendekezo kwa uongozi kuiangalia vyema idara hiyo ili kuepuka majeruhi wa muda mrefu katika kikosi chake . Anasadiki mfumo bora wa matibabu utapunguza lundo la majeruhi wa muda mrefu pia kuwajenga wachezaji katika saikolojia nzuri ya kucheza kwa moyo wote bila uoga wakijua kuna mfumo bora wa matibabu kikosini . Msimu wa 2016-17 Lwandamina amesumbuliwa sana na lundo la majeruhi kikosini mwake hivyo angependa hali hiyo isimkute msimu ujao.
Kocha huyo anaondoka ijumaa usiku kwenda likizo nchini Zambia na kufuatilia taratibu zingine za usajili akiwa huko na anatarajiwa kurejea nchini Juni 29 na kuanza maandalizi ya kikosi chake Julai 2 kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu.Facebook