Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amefungua mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi na Sekondari (UMISSETA na UMITASHUMTA) na kutoa agizo kwa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa somo la Haiba, Michezo na Stadi za Kazi kwenye shule za Msingi linafundishwa kikamilifu pamoja na kutenga fedha za kuendeshea michezo.
Akifungua Mashindano ya UMISSETA NA UMITASHUMTA katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana Mhe. Samia alisema ashindano ya UMISSETA na UMITASHUMTA yanatoa fursa ya kwa washiriki kuonyesha uwezo wa kuonekana kwa wadau mbalimbali ambao wataweza kuwaendeleza na kueleza kuwa zipo fursa nyingi za ajira endapo michezo na sanaa vitatumiwa vizuri na kwa ukamilifu kwa kuwa Michezo na Sanaaa ni ajira.
Ameongeza kuwa uhalali wa michezo na mashidano shuleni unatajwa katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015-2020 kipengele cha 161 kifungo kidogo cha (d) na kipengelea cha 161 kifungu cha (f), Sera ya Maendeleo ya michezo ya mwaka 1995 kifungu kidogo cha 2(b) kipengele cha 6, Sera ya Elimu ya mwaka 2014 kipengele cha 3.3.5 inaelekeza haja ya kutambua na kuendeleza vipaji vya wanafunzi shuleni, Dira ya Malengo ya Maendeleo ya 2015-20202 kipengele cha 3(i).
Aliwaeleza washiriki wa mashindano kuwa uwepo wao katika mashindano unawapa fursa ya kutambua uwezo walio nao kwa ukamilifu na kuzidi kujiwekea malengo ya maisha yao ya sasa na ya baadaye kwakuwa mashindano hayo ni sehemu ya kuwaandaa kuwa raia wema, wanaowajibika vyema katika masomo yao na wanaofahamu nafasi yao katika jamii wanayoishi kwa maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Alisema ukiwezesha michezo kwa wanafunzi wa ngazi zote kuanzia ngazi ya awali hadi Chuo Kikuu utakuwa umetambua kuwa michezo inasaidia kujenga afya za wanafunzi,.
“ Miili ikiwa na afya njea itabeba akili zilizo nzuri na imara ambazo zitasaidia kufanya vizuri kwenye mitihani ya masomo yao yote yakiwemo ya Sayansi na Sanaa na hatimaye kupata wataalamu waliosoma na ambao watatatumia utaalamu wao katika maendeleo ya viwanda nchini na hivyo kuliletea Taifa maendeleo kupitia michezo” Alisema Makamu wa Rais.
Aliwataka washiriki wa mashindano hayo kuonyesha Michezo na Sanaa yenye ushindani ulio na viwango bora na kuwaomba wanamichezo wote kucheza na kutambua kuwa hiyo ni nafasi ya kipekee ya kujenga urafiki miongoni mwao na kutekeleza kwa vitendo azma ya Taifa ya kuimarisha umoja mshikamano kati yao, jamii na taifa kwa ujumla.
Mhe. Suluhu alieleza kuwa Ushindani katika michezo ni zaidi ya ushindi au kupata medali na kuwataka washiriki kutumia mashindano hayo kuonesha uwezo wa vipaji walivyonavyo kindugu na kirafiki zaidi na kuendelea kuwa wamoja wakati wote kwakuwamichezo inafundisha ushindani unaoelekeza kukubali kushinda au kushindwa kwa matokeo yoyote na kuendelea kuwa wamoja.
Aliendelea kueleza kuwa Michezo ni zaidi ya kucheza na kwamba inafundisha washiriki kutenda majukumu yao katika nyanja mbalimbali kwa ushirikiano mwema bila kujali tofauti zozote zilizopo miongoni mwao.
Alisema endapo Taifa letu linataka kujenga msingi wa kupata matokeo bora ni lazima kuhakikisha kuwa vijana kuanzia shule za Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo wanatengenezewa mazingira na kupewa fursa zakucheza na kushidana miongoni mwao.”ni lazima kuwajengea vijana utamaduni endelevu wa kucheza ili kuendeleza vipaji, kupata wachezaji bora wa kuunda timu zetu zaTaifa za Michezo mbalimbali, kuwaandaa kwa maisha yao ya sasa na ya baadaye na kwa manufaa mapana ya Taifa kwani Matokeo mazuri yanapatikana kwa kufanya maandalizi ya kutosha na yenye tija.Alisisitiza Makamu wa Rais.
Kauli mbiu ya Michezo ya UMISSETA na UMITASHUMTA ya mwaka huu wa 2017 ni “ WEKEZA KATIKA MICHEZO KWA USTAWI WA ELIMU NA VIWANDA TANZANIA”.
Wakati huo huo, Makamu wa Rais ametaka kila mwananchi awe na utamaduni wa kufanya mazoezi ya viungo kwa ajili ya kuzuia magonjwa yasiyoambukiza na kila shule za msingi na sekondari wanafunzi wakimbie mchakamchaka kila siku kabla ya kuingia darasani, wanafunzi waimbe nyimbo za uzalendo wan chi yetu kila siku.
0 comments :
Post a Comment