IN SUMMARY
· Asifia uongozi wake na kwamba Watanzania wako salama chini ya Serikali yake
Dar es Salaam. Rais mstaafu wa awamu ya pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi amesema laiti Katiba isingekuwa na kipengele cha ukomo wa madaraka ya Rais, angeshauri Rais John Magufuli awe kiongozi wa siku zote kutokana na kazi kubwa anayoifanya ya kuwatumikia Watanzania.
“Kwa kuwa tuna Katiba basi hatuna budi kuifuata. Ila kikubwa Watanzania tuzidi kumuombea na kumsaidia Rais wetu”, alisema Mwinyi katika salamu zake za Eid el Fitr jijini Dar es Salaam jana.
Ibara ya 40(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 1984 inasema, “Bila ya kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika ibara hii, mtu yeyote ambaye ni Rais anaweza kuchaguliwa tena kushika kiti hicho.”
Hata hivyo, ibara ya 40(2) inasisitiza, “Hakuna mtu atakayechaguliwa zaidi ya mara mbili kushika kiti cha Rais.”
Ibara ya 38 ya Katiba hiyo imetaja vigezo vinavyompa fursa ya mtu fursa ya kugombea kuwa ni lazima awe na sifa zifuatazo: (a) ni raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano kwa mujibu wa Sheria ya Uraia; (b) ametimiza umri wa miaka arobaini; (c) ni mwanachama, na mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa; (d) anazo sifa za kumwezesha kuwa mbunge au mjumbe wa Baraza la Wawakilishi; (e) katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya Uchaguzi Mkuu hajawahi kutiwa hatiani katika Mahakama yoyote kwa kosa lolote la kukwepa kulipa kodi yoyote ya Serikali.
Ibara ya 38 inayozungumzia uchaguzi wa Rais inasema; (1) Rais atachaguliwa na wananchi kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii na kwa mujibu wa sheria itakayoweka masharti kuhusu uchaguzi wa Rais ambayo itatungwa na Bunge kwa kufuata masharti ya Katiba hii.
Aya ya pili ya ibara hiyo imeainisha namna mkuu huyo wa nchi anavyoweza kuondolewa na kuondoka maradakani ikisema, “Bila ya kuathiri masharti mengineyo ya Katiba hii, kiti cha Rais kitakuwa ki wazi, na uchaguzi wa Rais utafanyika au nafasi hiyo itajazwa vinginevyo kwa mujibu wa Katiba hii, kadri itakavyokuwa, kila mara litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo; (a) baada ya Bunge kuvunjwa; (b) baada ya Rais kujiuzulu bila ya kulivunja Bunge kwanza; (c) baada ya Rais kupoteza sifa za kushika nafasi madaraka ya kuchaguliwa; (d) baada ya Rais kushtakiwa Bungeni kwa mujibu wa Katiba hii, na kuondolewa katika madaraka; (e) baada ya kuthibitishwa kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37 ya Katiba hii kwamba Rais hawezi kumudu kazi na shughuli zake; (f) baada ya Rais kufariki.
Hata hivyo, aya ya 3 inasema kiti cha Rais hakitahesabiwa kuwa kiwazi kwa sababu tu ya Bunge kupitisha hoja ya kutokuwa na imani kwa Waziri Mkuu.
Mwongozo wa Uchaguzi Mkuu ambao pia unashirikisha ule wa Rais, wabunge na madiwani kwa upande wa Jamhuri ya Muungano uliweka ukomo na sifa mpya za wagombea baada ya kung’atuka madarakani kwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1985.
Mwalimu Nyerere ndiye aliyeongoza nchi kwa muda mrefu kuanzia Oktoba 29, 1964 hadi Novemba 5, 1985 alipomkabidhi Rais Mwinyi. Kabla ya Tanganyika na Zanzibar kuungana na kuwa Rais wa Tanzania, Nyerere aliongoza Serikali ya Tanganyika kwa miaka mitatu na miezi 11. Hata hivyo, tangu kuondoka kwake maradakani, waliomfuata hawakung’ang’ania madaraka pale muda wao wa miaka 10 ya kikatiba ulipomalizika.
Kauli ya Mwinyi
Akizungumza jana wakati akitoa salamu za Eid el Fitr muda mfupi baada ya kushiriki ibada ya sikukuu hiyo iliyofanyika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Mwinyi ambaye aliongoza nchi kuanzia mwaka 1985 hadi 1995, alisema kazi kubwa inafanywa na Serikali ya sasa chini ya kiongozi wake, Dk Magufuli.
Mwinyi maarufu kama ‘Mzee Ruksa’ alisema Rais Magufuli amefanya kazi kubwa ya kuwaongoza wananchi na kwamba nchi imetulia na mahitaji wanayoyataka watu, mkuu huyo wa nchi anayatimiza na kuwalinda Watanzania ili waheshimiwe.
“Kwa kuwa tuna Katiba, basi hatuna budi kuifuata. Ila kikubwa Watanzania tuzidi kumuombea na kumsaidia Rais wetu”, alisema na kuongeza.
“Waswahili wanasema ‘kidole kimoja hakivunji chawa’. Naomba tuendelee kushikamana na kushikana kumsaidia Rais kama Sheikh wa Mkoa (Alhad Mussa Salum) alivyosema,” alisema Mwinyi.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Hussein Mwinyi; Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), Seleman Jafo na Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba.
Kwa upande wake, Dk Hussein Mwinyi aliwataka Watanzania kuendelea kudumisha matendo waliyofanya katika mwezi wa Ramadhan na Serikali itazidi kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo mbalimbali ikiwamo Kibiti.
“Vyombo vya dola vinaendelea kuimarisha ulinzi na kwamba mimi mwenyewe nitakwenda huko (Kibiti) kwa sababu ni sehemu yangu ya kazi,” alisema Dk Mwinyi.
Akizungumza katika sala hiyo ya ya Eid, Profesa Lipumba aliwataka Watanzania kuimarisha umoja na mshikamano na washerehekee kwa amani na utulivu.
Kabla ya viongozi hao kuzungumza, Sheikh Alhad alisema Rais Magufuli analinda rasilimali za nchi na anataka kila Mtanzania afaidike na rasilimali za Taifa.
“Waumini wa dini zote tushikamane ili kuilinda nchi. Rais Magufuli ana kazi kubwa ya kuwatumikia Watanzania, hivyo mshikamano unahitajika zaidi,” alisema Sheikh Alhad na kuongeza kuwa:
“Tanzania ni nchi ya amani na viongozi wake ni watulivu na wanamsaidia Rais Magufuli. Kila Rais ana awamu yake na sasa hivi ni awamu ya Rais Magufuli.
0 comments :
Post a Comment