*TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI NA UMMA*
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Lowassa amepata wito kutoka kwa Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) kumtaka kufika Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kesho Jumanne, saa 4 asubuhi kwa ajili ya mahojiano.
Mhe. Lowassa ambaye pia alikuwa Mgombea Urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) kupitia CHADEMA, kwenye Uchaguzi Mkuu uliopita, hajapewa maelezo wala ufafanuzi wowote kuwa mahojiano hayo yatahusu nini hasa.
Tayari Chama kimetoa maelekezo kwa Kurugenzi ya Katiba na Sheria ya Chama kuhakikisha kuwa Mhe. Lowassa anapata msaada wa kisheria wakati wa mahojiano hayo.
Taarifa za awali zinaonesha kuwa mahojiano hayo yanahusishwa na kauli za Mhe. Lowassa alizotoa katika nyakati tofauti hivi karibuni wakati akishiriki futari pamoja na Watanzania wenzetu Waislam waliokuwa katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhan, ambapo amekuwa kiitaka Serikali kuzingatia misingi ya utawala bora kama mojawapo ya misingi muhimu ya kuendesha nchi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Watanzania wote.
Imetolewa leo Jumatatu, Juni 26, 2017 na;
*Tumaini Makene*
*Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano*
*CHADEMA*
0 comments :
Post a Comment