TUME ya Utumishi wa Walimu imesema mwalimu ambaye hataonekana katika kituo chake cha kazi kwa siku tano bila taarifa, atakuwa amejifukuzisha kazi na hakutakuwa na mjadala katika hilo.
Pia imewaonya walimu wenye tabia ya kufanya mapenzi na wanafunzi na kuwapa ujauzito, watakaobainika kufanya hivyo watafukuzwa kazi na hawataweza kuajiriwa popote. Amewaonya walimu wa kike wanaotamani wanafunzi wa kiume kuwa huo ni sawa na uchawi.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu wa Tume ya utumishi wa Walimu Taifa, Winifrida Rutaindurwa wakati wa kuapishwa kwa wajumbe wa tume hiyo wa Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma iliyoambatana na uzinduzi wa mkakati wa kuboresha nidhamu na kuinua taaluma.
Uzinduzi huo wa kitaifa umefanyika kwa kuwakilisha wilaya nyingine 138 nchini. “Mtu akikosa kazini siku tano bila taarifa au ruhusa adhabu yake ni kufukuzwa kazi hakuna mjadala wala kuhurumiana,” alisema.
Alisema watumishi hao watoro wamekuwa wakiitia hasara serikali kwa sababu mashauri yao yanahitaji fedha katika kuyashughulikia. Alisema mpaka sasa kuna mashauri 1,200 ambayo ni viporo na hiyo inatokana na walimu kutozingatia sheria na kanuni.
Pia alisema wale wote watakaobainika kuwa ni wabadhirifu watafukuzwa kazi na hata wakipatikana wanaendesha biashara ya pikipiki muda wa kazi adhabu iliyopo ni kufukuzwa kazi. Alisema baadhi ya walimu wamekuwa wakiomba ruhusa ya kusoma miaka mitatu lakini wanapomaliza wanaamua kuendelea tena na masomo bila kupata kibali cha mwajiri.
“Tumepata taarifa nyingi watoto wa kike wanapata mimba za walimu, acheni kutamani wanafunzi kama unapenda sare mshonee mkeo, ukikutwa na kosa hilo utafukuzwa kazi na hutaajiriwa popote,” alisema. Alisema kumekuwa na tabia ya walimu wa kike kutamani watoto wa kiume.
“Huo ni sawa na uchawi unatafuta nini kwa mtoto mdogo,” alisema. Katibu Msaidizi wa tume hiyo Wilaya ya Chamwino, Khalid Shaban alisema kuanzia mwakani wataanza kutoa tuzo ili kuongeza mori ya kazi na watahakikisha kila mwalimu mwenye sifa na vigezo anapata haki yake.