WATU wawili wamekufa na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali iliyotokea baada ya basi la Kampuni ya Upendo kuacha njia na kupinduka.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, Augustino Senga alisema ajali hiyo ni ya juzi saa mbili asubuhi katika eneo la Mlomboji Kata ya Igawa, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali.
Alisema basi hilo lenye namba za usajili T 543 CSF aina ya HIGER, lililokuwa likiendeshwa na Ramadhani Mohammed (35) mkazi wa Dar es Salaam, lilikuwa likitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam.
Alitaja abiria waliokufa kuwa ni Emmanuel Obeid (30) mkazi wa Chimala, Mbarali na mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Shaibu, anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 35 na 40.
Alitaja waliojeruhiwa ni Esau Sanga (43) mkazi wa wilayani Makete mkoani Njombe, Frank Ngimbe (21), Tukumbekege Mwakyusa (60) na Jena Michael (26), wote wakazi wa jijini Mbeya.
0 comments :
Post a Comment