Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imefanya mabadiliko ya Kamati ya Uchaguzi na kuwaengua wajumbe wanne walioonyesha kumtetea Rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi ambaye kwa sasa yuko rumande kwa tuhuma mbalimbali.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Kikao cha Kamati ya Utendaji ya TFF kilichofanyika leo mchana makao makuu ya shirikisho hilo zilizopo katika Uwanja wa Karume, Ilala, Dar es Salaam chini ya Kaimu Rais, Wallace Karia.
Wajumbe walioondolewa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti, Wakili Domina Madeli, Juma Lallika, Jeremiah Wambura na Hamim Mahmoud Omar na sasa Mwenyekiti, Wakili Revocatus Kuuli atafanya kazi na Mbunge wa Rufiji, Mohamed Mchengerwa, Wakili Malangwe Ally Mchungahela, Wakili Kiomoni Kibamba ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na Wakili Thadeus Kalua.
Kabla ya hapo, Mwenyekiti Kuuli alitofautiana na Wajumbe wenzake wote wa Kamati hiyo ya awali juu ya Malinzi kuruhusiwa kuendelea kugombea katika uchaguzi wa Agosti 12, mwaka huu mjini Dodoma licha ya kwamba hakutokea kwenye usaili.
Kamati nyingine zilizotajwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi leo ni Kamati ya Maadili ambayo inaundwa na Mwenyekiti, Hamidou Mbwezeleni, Steven Zangira, Mkuu wa Wilaya ya Tarime mkoani Mara, Glorius Luoga, Walter Lungu na Amin Bakhresa.
Kamati ya Rufaa ya Maadili; Wakili Rugemeleza Nshala, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, DCP Mohammed Mpinga, Wakili Benjamin Karume, Dkt Lisobine Chisongo, ASP Benedict Nyagabona.
Kamati ya Nidhamu; Tarimba Abbas, Peter Hela, Boniface Lyamwike, Dkt Billy Haonga na Kassim Dau.
Kamati ya Rufaa ya Nidhamu; Wakili Rahim Zubeiry Shaaban, Siza Chenga, Abbas Mtemvu, Amani Mulika na Stella Mwakingwe wakati Kamati ya Rufaa ya Uchaguzi ikiundwa na Wakili Abdi Kagomba, Kenneth Mwenda, Rashid Sadallah, Jabir Shekimweri na Mohamed Gombati.
0 comments :
Post a Comment