Kinachoendelea Kuhusu swala la Halima mdee kuwekwa mahabusu


Hadi sasa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama, Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee bado anashikiliwa na Jeshi la Polisi, Kituo cha Polisi Oysterbay, takriban masaa 72 tangu alipokamatwa na kuwekwa ndani kwa masaa 48 kwa maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni.

Kwa mujibu wa Mawakili wa Chama wakiongozwa na Peter Kibatala, ambao wamekuwa wakifuatilia hatma ya Mhe. Mdee tangu ilipotolewa amri ya kukamatwa kwake, wanasema polisi wanaendelea kumshikilia Mhe. Mdee kwa ajili ya mahojiano ambayo hadi jioni hii haijaelezwa yatahusu tuhuma zipi.

Mahojiano hayo ambayo leo yameshindikana kufanyika kwa siku nzima kwa kile kilichoelezwa kuwa RCO ambaye ofisi yake ilikuwa na jukumu la kumhoji Mhe. Mdee alikuwa katika shughuli zingine ikiwa ni pamoja na kuwa kikaoni Makao Makuu ya Jeshi la Police.

Msimamo wa chama

Tunaendelea kusisitiza msimamo ambao tayari tumeshautoa kuwa Chama kinakusudia kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambao wamekuwa wakitumia vibaya madaraka yao hasa kupitia *Sheria ya Tawala za Mikoa* kudhulumu na kuminya haki za wananchi mbalimbali wakiwemo wanachama na viongozi wa CHADEMA kwa kuwaweka ndani kwa msaa 48, kinyume cha sheria za nchi na tayari kimeshawaagiza wanasheria kuanza mchakato kwa ajili ya hatua hizo.

Suala la Mhe. Mdee ambaye kuanzia kutolewa kwa amri ya kukamatwa kwake, kukamatwa, kuwekwa ndani kwa masaa 48 na kuendelea kuwa ndani hadi sasa ni kinyume kabisa cha sheria, utakuwa ni mojawapo ya mifano itakayotumiwa na chama kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wakuu hao wa mikoa na wilaya.

Kutokana na matukio kadhaa ya namna hiyo ya matumizi mabaya kabisa ya madaraka, yakiwemo ya hivi karibuni kama lile la DC wa Kinondoni aliyetoa amri ya kuwekwa ndani kwa Mstahiki Meya Boniface Jacob na hili la sasa la Mhe. Mdee, chama kinaamini Mahakama itatoa tafsiri sahihi ya matumizi ya Sheria ya Tawala za Mikoa inayotumiwa na maRC na maDC vibaya 'kuhukumu na kuwafunga watu masaa 48' kinyume kabisa na sheria.

Mhe. Mdee mwenyewe pia kupitia kwa wanasheria wake, ameonesha nia ya kuchukua hatua za kisheria kukomesha tabia hiyo kwa kulifikisha suala hilo mahakamani na kulisimamia hadi mwisho kwa ajili ya kukomesha vitendo hivyo visifanywe tena na maRC au maDC kwa watu wengine. Aidha anakusudia pia kuiomba mahakama itoe tafsiri sahihi ya kitendo cha kufungwa kinyume cha sheria (unlawfully imprisonment) kama alivyofanyiwa yeye.

Tumaini Makene
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment