Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amemwita kikosini kinda Athanas Mdamu ambaye ni mchezaji mwanafunzi kutoka Shule ya kukuza vipaji ya Alliance ya Mwanza.
Mayanga amemuita nyota huyo anayekipiga katika timu ya Alliance inayoshiriki ligi daraja la kwanza, ili kumpatia uzoefu kwenye timu ya taifa ya wakubwa na ataungana na timu huko huko jijini Mwanza yaliko makazi yake.
Taifa Stars ambayo imerejea nchini usiku wa kuamkia leo , inajipanga kwenda Mwanza siku ya Jumatatu kujiandaa na mchezo dhidi ya Rwanda unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Julai 15 mwaka huu ukiwa ni mchezo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN).
Wachezaji wanne hawatakuwako kwenye kikosi ambao ni majeruhi Mbaraka Yussuf na Shaban Idd Chilunda kadhalika nyota wa kimataifa ambao hawahusiki na mechi za CHAN ambao ni Thomas Ulimwengu na Elius Maguri
Tayari Mayanga amewaongeza nyota wawili katika kikosi hicho ambao ni John Bocco na Kelvin Sabato kutoka Majimaji ya Songea kujaza nafasi za Chilunda na Mbaraka.
Timu hiyo ambayo kwa mwaka huu imecheza mechi tisa za kimataifa na kushinda mitano; kutoka sare miwili na kufungwa mmoja wa nusu fainali za Cosafa, itakuwa na kikosi cha wachezaji 20.