Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA limelifungia Shirikisho la mpira wa miguu Sudani (SFA) kuanzia tareh 6 Julai kutokana na Serikali ya nchi yao kuingilia shughuli za shirikisho la nchi hiyo kinyume na taratibu za FIFA.
Shirikisho la Sudani (SFA) limekutana na dhahama hiyo baada ya Serikali ya Sudani kupitia wizara yake ya Sheria kuamuru Rais anaetambuliwa na FIFA Mutasim Gaafar kuondoka madarakani na nafasi yake ichukuliwe na Rais mpya Abdel Rahman Sir Elkatim kinyume na taratibu za soka.
Tarehe 27 Juni, FIFA iliiomba Serikali itengue agizo lake na kumrudisha madarakani Raisi aliyeondolewa tarehe 2 juni kabla ya mwisho wa mwezi wa Sita lakini Serikali ilikataa kufanya hivyo.
Kutokana na hatua hiyo timu ya Al-Hilal, Al Merreikh, Al-Hilal Obeid pamoja na timu ya taifa ya Sudan hazitoweza kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa mara tu baada ya kufungiwa kwa SFA.
Mechi baina ya Etoile du Sahel ya Tunisia dhidi ya Al-Merreikh ya Sudani iliyokuwa inatazamiwa kuchezwa leo na kuoneshwa na ZBC 2 haitokuwepo na badala yake, utaletewa mechi kati ya Zamalek ya Misri dhidi ya Al-Ahli Tripoli ya Libya itakayopigwa tarehe 9 Julai