Siku moja baada ya Jeshi la Polisi kuwaua watu sita wanaodaiwa kuwa majambazi na wengine wawili kukimbia katika Mtaa wa Fumagila Mashariki Kata ya Igoma wilayani Nyamagana jijini Mwanza, taharuki imeendelea kuwakumba wananchi wa eneo hilo wakihofu kuwa huenda wakarudi.
Akizungumza  leo Jumapili, Julai 9, Mwenyekiti wa mtaa huo, William Ngemela amesema tukio hilo limetoa elimu tosha katika mtaa huo na mitaa jirani huku akidai tangu azaliwe hajawahi kushuhudia tukio kama hilo.
“Hii ni elimu tosha kwasababu haya yote hatukutegemea kama yanaweza kutokea kwenye mtaa kama huu, lakini angalia silaha zote na vitu vilivyokamatwa, kwakweli inatishia amani,” amesema Ngemela.
Katika tukio hilo polisi walikamata silaha ya SMG AK47, magazine mbili kila moja ikiwa na risasi 30, risasi 36 za AK 47ambazo zilikuwa nje ya magazine, risasi moja aina ya rafal, risasi nane za shortgun.
Silaha nyingine ni bastola nne za kienyeji, sare za jeshi za nchi jirani, kofia sita za kuziba uso, kitambaa cha kichwani, nusu kanzu, nguo mbalimbali za kiume, mabegi matatu yaliyokuwa yakihifadhi silaha hizo, baiskeli mbili, pikipiki moja, unga na dagaa.
Mwenyekiti huyo amesema watu hao walikuja mtaani hapo kama waumini wa dini ya kiislamu kumbe walikuwa na mambo yao, lakini hili limekuwa fundisho kwetu ni wajibu wetu wote kushirikiana, mimi ni mwenyekiti mmoja lakini jamii ninayoingoza ni kubwa inapaswa kutoa taarifa.”
Amesema tangu lilipotokea tukio hilo jana, baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawakutoka nje ya nyumba zao walijifungia wakiogopa kuwa hao waliokimbia wanaweza kurudi kufanya jambo baya, kwahiyo hali bado haijawa nzuri kwa wakazi wangu.”
Ishmael John, mkazi wa mtaa wa Kanenwa, alisema, “kiukweli hatuwezi kuwa na amani ya
kutosha kutokana na jinsi hali ilivyokuwa juzi.”
Mkazi mwingine wa mtaa huo, Robert Musabi amesema itakuwa vigumu kuamini kwamba hali itakuwa salama hususani ukizingatia baada ya wawili kukimbilia kusikojulikana.
Hata hivyo mwenyekiti wa mtaa wa Kanenwa jirani na mtaa huo, James Buduma amesema serikali za mitaa eneo hilo tayari zimeanza kutekeleza agizo la mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella la kusajili kila mtu ambaye anafika akiwa mgeni na ajitambulishe uhalisia wake.
Kamanada wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi amesema zoezi hilo la kuwasaka wahalifu ni endelevu na hakuna atakayesalimika katika operesheni hiyo hivyo kuwataka wanaofanya vitendo hivyo waache mara moja.