Jeshi la Polisi limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wakazi wa bonde la mto Msimbazi waliokuwa wakipinga kubomolewa makazi yao na kuwakamata watu takriban 20 wakihusika na vurugu hizo.
Tukio hilo limetokea leo, Jumatano kufuatia utekelezaji wa zoezi la bomoabomoa linalofanywa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, tayari kwa matayarisho ya kupisha mradi mkubwa wa majitaka katika manispaa hiyo.
Wakazi wa eneo hilo wamelalamikia zoezi hilo na kuiomba Serikali kuwaonea huruma kwani hawana mahali pengine kwa kwenda kujisitiri.
Licha ya maombi hayo, hata hivyo serikali kupitia uongozi wa jiji ulishapiga marufuku eneo hilo la Jangwani kuendelezwa kwa makazi kutoka na kuwa miongoni mwa maeneo hatarishi wakati wa msimu wa mvua za masika kutokana na uwepo wa mkondo wa mto Msimbazi.
Vurugu zilizoibuka wakati wa kuvunja vibanda katika bonde la Jangwani zimesababisha basi na kituo cha Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Udart) kuvunjwa vioo kwa mawe.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Udart, Deus Bugaywa amesema bado hawajafanya tathmini kujua thamani ya mali iliyoharibiwa.
Akizungumzia uvunjaji wa vibanda hivyo ulifanyika leo Jumatano, msemaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (Dawasa), Nelly Msuya amesema umetekelezwa na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ili kuwapisha Dawasa kujenga mtambo wa maji taka.



0 comments :
Post a Comment