Humphrey Polepole amefunguka na kusema Rais Magufuli hakuwahi kuwa na nafasi ya uongozi ndani ya Chama hicho na kudai ndiye alikuwa mtu sahihi 2015 kwani alipoingia ndani ya chama na serikali ameweza kuona matatizo ambayo wengine hawakuweza kuyaona.
Polepole amesema kuwa kwa jinsi ambavyo chama hicho kilivyokuwa kipindi cha nyuma kilihitaji mtu ambaye hayupo ndani ya mfumo wake ili aweze kuona mapungufu mbalimbali ndani ya chama na serikali.
“Ndugu Magufuli kama Mwenyekiti ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) amekuwa ni kiongozi wa kawaida na duniani kote unaposoma elimu ya mageuzi huwa inataka upate mtu ambaye ni wa kawaida labda huenda asiyetoka katika eneo ambalo linafanyiwa mageuzi ili aweze kuwa na jicho la nje, kwa sababu gani wewe unayekaa ndani unaona kama mambo yako sawa hivi, sasa ndugu Magufuli ndani ya CCM hajawahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu, hajawahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, hajawahi kuwa Mjumbe wa Sekretarieti sasa CCM ilipotafakari ni nani atakayeweza kufanya mageuzi makubwa ndani ya chama hivyo hakukuwa na mtu mwingine zaidi ya John Pombe Magufuli” alisema Polepole
Aidha Polepole amesema kuwa Rais Magufuli alipoingia serikalini na ndani ya Chama Cha Mapinduzi hakuona haya kusema madudu na uozo uliopo ndani yake
“Magufuli hajaona haya kusema kwanini dhahabu inaondoka mnaitazama, Kwanini hii Almasi inakwenda na kwanini tunashindwa kuichakata hapa, kwanini bandarini mnaruhusu mizigo inaingia bila kulipa kodi, na nyinyi CCM kwanini mali zenu zinahodhiwa na watu na fedha haziji kwenye chama, hii yote ni kwa sababu anajicho la nje ambaye anaona tofauti na nyinyi mliopo ndani ya ambao mshazoe”alisema Polepole
Mbali na hilo Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema kuwa anapomsikia Rais Magufuli akisema kuwa nafasi ya Urais ni kazi ngumu anamuelewa kweli na kusema kuwa yeye anajua uongozi si kazi ya furaha bali ni mzigo mkubwa.FacebookTwitterGoogle+Share