Wednesday, December 20, 2017
Bunge la Afrika Mashariki (Eala) limemchagua Spika kutoka Rwanda, Dk Martin Ngoga katika uchaguzi ulioibua mabishano ya kisheria juu ya uhalali wa kufanyika kwake.
Baada ya dua ya kuliombea Bunge, mbunge Dk Ngwaru Maghembe kutoka Tanzania aliomba mwongozo wa kuliahirisha kutokana na akidi kutotimia kutokana na wabunge tisa wa Burundi na saba wa Tanzania kutokuwepo kwa sababu ambazo hazikujulikana.
Mbunge kutoka Uganda, Freddy Mbidde alipinga hoja hiyo akisema kanuni ya 53(1) inayozungumzia akidi inahusu Bunge rasmi ambalo tayari lina Spika lakini kwa kuwa hawakuwa na Spika kanuni hiyo haina nguvu kisheria.
Mbunge mwingine wa Tanzania, Dk Abdullah Makame alisema kutokana na Bunge kuchelewa kuanza kazi kwa kipindi cha miezi sita kutokana na mwanachama wa EAC nchi ya Kenya kuchelewa kuchagua wabunge ni busara uchaguzi usifanyike hadi wabunge wote wawepo.
Hoja hiyo ilipingwa na mbunge kutoka Uganda, Suzane Nakauki aliyedai hoja ya kutokufanya uchaguzi kwa sababu ya wabunge kutokuwepo haina mashiko kisheria na kikanuni kwa sababu wameorodhesha majina yao kwenye kitabu cha mahudhurio na wamepewa posho na wameamua kwa sababu zisizojulikana kugomea uchaguzi.
Alisema haiwezekani wabunge wa Tanzania ambao wapo nchi mwao washindwe kuhudhuria kikao cha Bunge wakati wapo jijini Arusha, huku waliotoka mbali wakiwepo.
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Balozi Liberat Mfumukeko alisema kila jambo lenye mgogoro kwenye mihimili ya EAC lina utaratibu wa kulimaliza kwa njia ya kuomba ushauri kwa sekretariati, Mahakama, baraza la mawaziri na kikao cha marais.
Hatua hiyo ilimwinua Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi, Isabella Ndahayo aliyesema wabunge wa Burundi hawakuridhishwa na utaratibu wa uchaguzi licha ya kanuni kutamka wazi nafasi ya Spika ni ya mzunguko kwa nchi wanachama.
"Wabunge wa Burundi hawapo kwa sababu hawaridhiki na kinachoendelea, naomba tupewe tafsiri ya nafasi ya Spika kuwa ni mzunguko kwa nchi wanachama, si kwamba tunapinga juhudi za mshikamano wa jumuiya bali tafsiri halisi," alisema Isabella.
Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Uganda ambayo ni Mwenyekiti wa EAC, Julius Wandera alisema kumekuwa na mashauriano kati ya baraza la mawaziri wa jumuiya hiyo ili kuhakikisha suala hilo linakamilika.
Baada ya mabishano ya kisheria na kanuni, katibu wa bunge aliamua uchaguzi kufanyika na awamu ya kwanza, mgombea kutoka Rwanda, Dk Martin Ngoga alipata kura 35, Leontine Nzeyimana wa Burundi kura moja na Adam Kimbisa wa Tanzania hakupata kura.
Kutokana na kanuni kuhitaji mshindi kupata theluthi mbili ya kura zote 52, uchaguzi ulirudiwa kwa kanuni ya mshindi kupatikana kwa wingi wa kura na Dk Ngoga aliibuka mshindi kwa kupata kura 33 dhidi kura tatu za Nzeyimana ambaye hakuwepo bungeni.
Baada ya kula kiapo Dk Ngoga ambaye alikuwa mwendesha mashtaka mkuu wa Rwanda alisema anafahamu uchaguzi wowote lazima uache majeraha lakini yupo tayari kushirikiana na kila mbunge kujenga jumuiya hiyo.
0 comments :
Post a Comment