Tahadhari Mvua Kubwa Yatarajiwa Kunyesha Mikoa Minne

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), imesema wakati wa kuelekea sikukuu za Krismasi na mwisho wa mwaka, mvua kubwa zinatarajia kunyesha katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Kigoma.

Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri wa Hali ya Hewa wa TMA, Samuel Mbuya, aliieleza Nipashe jana kwa njia ya simu kuwa, maeneo ya ukanda wa Pwani zinakoendelea kunyesha mvua ni zile za kumalizikia msimu wa vuli.

Alisema mikoa hiyo minne ndio inatarajiwa kuwa na mvua wakati wa sikukuu na ifikapo mwisho wa mwezi huu, mvua za vuli zinazoendelea kunyesha mikoa mbalimbali ikiwamo Dar es Salaam zitakuwa zimefikia ukingoni.

“Mvua zinazonyesha maeneo ya ukanda wa Pwani ni zile za vuli na zilianza Oktoba na zinaisha mwisho wa mwezi huu, si mvua zinazoendelea isipokuwa tu katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Rukwa na Kigoma ambako katika msimu huu wa sikukuu kutakuwa na mvua,” alisema.

Pia, alisema TMA inatarajia mvua zitaendelea kunyesha katika maeneo ya mikoa ya Magharibi ambayo ni Kigoma, Tabora, Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Lindi, Dodoma na Singida.

Alisema mvua katika ukanda huo zilianza kunyesha Novemba na zinatarajiwa kumalizika Aprili.

Mbuya alisema maeneo mengine katika mikoa hiyo kutakuwa na mvua za kawaida huku mikoa minne ikiwa na mvua kubwa.

Aliwataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA mara kwa mara, zinazowapa mwelekeo wa hali ya hewa na tahadhari wanazotakiwa kuchukua.

Kadhalika, alisema wananchi wanapopata taarifa wanatakiwa kuchukua tahadhari mapema ili kuondokana na madhara yanayoweza kutokana na mvua hizo.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment