Bomoa bomoa Moshi

Maofisa mipango miji na askari wa Manispaa ya Moshi wameanza kusimamia ubomoaji wa majengo ya biashara yaliyojengwa na kukarabatiwa kinyume cha sheria.
Ujenzi huo uliofanywa chapuchapu kati ya Desemba 23 na Desemba 26,2017 katika kata za Kiusa, Bondeni na Mawenzi, ulifichuliwa na gazeti la Mwananchi na kusababisha madiwani kupaza sauti wakitaka majengo hayo yavunjwe.
Kwa mujibu wa sheria za mipango miji na mpango kabambe wa mji wa Moshi, inakatazwa kukarabati majengo ya zamani au kujenga mapya ambayo si ya ghorofa katika kata hizo.
Leo Jumatano Januari 3,2018 kuanzia saa tatu asubuhi, maofisa mipango miji na askari wa mji walifika katika moja ya nyumba hizo iliyojengwa upya bila vibali vya halmashauri wakiwataka wabomoe au manispaa ibomoe.
Baada ya mazungumzo, wamiliki wa jengo hilo lililopo barabara ya Sokoni karibu na hosteli ya Umoja waliokataa kuzungumza na wanahabari walikubali kubomoa wakianzia kuondoa mabati.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mipango Miji ya Halmashauri ya Manispaa ya Moshi, Tonny Ndewawio alisema ujenzi na ukarabati wa majengo hayo haukuwa na kibali na hauruhusiwi kisheria.
“Halmashauri tulishapeleka stop order (amri ya zuio) na baadaye tukapeleka demolishing order (amri ya kuvunja) hawakufanya hivyo. Watendaji sasa ndiyo kazi yao kusimamia uvunjaji,” amesema Ndewawio.
Mwenyekiti huyo ameyataja maeneo mengine ambayo yamekarabatiwa na kufunguliwa fremu za maduka kuwa yapo kata za Bondeni, Mawenzi na Kiusa, akisema pia yatafikiwa.
Wiki iliyopita, Meya wa Manispaa ya Moshi, Raymond Mboya aliliambia gazeti la mwananchi kuwa kilichofanyika ni ukiukwaji wa utaratibu ambao uko wazi na kwamba, hakuna kibali kilichotolewa kuruhusu ujenzi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment