Kilichowaponza Yanga Kutolewa Mapinduzi Cup Hiki Hapa

UMAKINI wa safu ya kiungo na ulinzi ya timu ya URA uliiwia vigumu mabingwa wa soka nchini Yanga kuweza kupata ushindi kwenye dakika 90 za mchezo wa nusu fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi.
Yanga inayodhaminiwa na kampuni ya Sportpesa jana ilitolewa kwenye michuano hiyo, baada kufungwa kwa penalti 5-4 na Waganda hao ambao sasa wametinga hatua ya fainali.
Pamoja na kumiliki mpira kwa asilimia 56, Yanga walikosa mbinu ya kuipita ngome ya ulinzi ya URA licha ya mashambulizi waliyoyafanya katika kipindi cha kwanza.
URA imeendelea kuwa mwiba kwa timu za Tanzania baada ya kuzifunga Azam FC na Simba kwenye hatua ya makundi kabla ya kuifunga Yanga jana.
Wafungaji wa penalti kwa upande wa Yanga ambayo jana Kocha wake Mkuu, George Lwandamina aliishuhudia timu yake akiwa jukwaani,  walikuwa ni Papy Tshishimbi,  Hassan Kessy,  Raphael Daudi na Gabriel Michael, huku Obrey Chirwa akikosa penalti ya mwisho.
Penalti za URA zilifungwa na Kalama Deboss,  Kibumba Enock, Kagimu Shafik,  Kulaba Jimmy na Brian Majwega.
KIPINDI CHA KWANZA
Kipindi cha kwanza kilianza kwa URA kuwahi kufika langoni mwa Yanga katika dakika ya kwanza tu ya kipindi hicho, lakini shuti la mshambuliaji Bokota Labama lilitoka nje ya lango la Yanga.
Winga Kagamba Nicholas wa URA aliachia shoti dakika ya pili, lakini kipa wa Yanga, Youthe Rostand alilipangua na kuwa kona tasa.
Huku timu zote zikisoma, dakika  ya tisa  kiungo wa Yanga aliachia shuti kali langoni mwa URA akiwa nje ya 18, lakini liliwababatiza mabeki wa URA kabla ya kipa kudaka.
Kuanzia dakika ya 15, Yanga ilitawala mchezo, lakini kama ilivyokuwa dakika za mwanzo kwa URA, nayo haikuwa na mipango mizuri ya kutengeneza bao.
URA walirudi langoni mwa Yanga dakika ya 24 ila Rostand alikuwa makini na kulicheza shuti la Deboss.
Kama Yanga ingekuwa makini dakika ya 33 ubao wa matangazo kwenye uwanja wa Amaan mjini hapa ungeweza kubadilika,  lakini Ibrahimu Ajibu na Juma Mahadhi walijichanganya katika kuuwahi mpira mrefu uliopigwa na Hassan Kessy hivyo kumpa nafasi kipa Alionzi Nafian kudaka kirahisi.
Kipindi cha pili URA walianza tena kwa kasi na katika dakika ya kwanza ya kipindi hicho ilifanya shambulizi kali, lakini Rostam alikuwa makini kuokoa hatari.
Katika dakika ya 49 hadi ya 52 Yanga iliweka kambi langoni mwa URA na kupata kona tatu, lakini hazikifanikiwa kuzaa matunda.
 Licha ya Yanga kufanya mabadiliko katika dakika ya 53 kwa kumtoa Buswita na kumuingiza Obrey Chirwa bado hakukusaidia timu hiyo kupata bao.
URA sasa itacheza fainali na mshindi wa mchezo wa jana usiku kati ya Azam FC dhidi ya Singida United.
 Vikosi Yanga: Youthe Rostand, Hassan Hamisi, Mwinyi Haji,  Andrew Vicent, Kelvin Yondani,  Said Juma, Pius Buswita,  Papy Tshishimbi, Juma Mahadhi,  Ibrahim Ajibu,  Emmanuel Martin
URA: Alionzi Nafian,  Kibumba Enoch,  Majwega Brian,  Munaamba Allan,  Mbowa Patrick,  Mutyaba Julius,  Kagaba Nicholas,  Kalama Deboss, Bokota Labama,  Kagimu Shafik,  Ssempa Charles.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment