Odinga Ajiapisha Kuwa Rais Wa Jamuhuri Watu Wa Kenya ,Hatihani Kushtakiwa Kwa Uhaini

 
MAMLAKA za Kenya, jana zilizima vituo vya televisheni kuzuia matangazo 'live' ya sherehe za kuapishwa kwa kiongozi wa upinzani, Raila Odinga, ambaye alisusia uchaguzi wa marudio wa mwaka jana uliobishaniwa. 
Alijitangaza kuwa "rais wa watu" mbele ya maelfu ya wafuasi wake katika mji mkuu wa Nairobi.
 
Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Agosti, mwaka jana, yalibatilishwa kutokana na  madai ya ukiukwaji wa kanuni.
 
Uhuru Kenyatta alishinda uchaguzi wa marudio Oktoba, lakini Odinga hakushiriki, hivyo Kenyatta aliapishwa kuongoza muhula wa pili Novemba, mwaka jana.
 
Alivionya vyombo vya habari kutotangaza shughuli ya jana na mwanasheria wa serikali alisema kufanya hafla hiyo ni kosa la uhaini.
 
Hata hivyo, vituo vikuu vya TV vilionyesha tukio hilo kupitia mitandao yake ya kompyuta, kwenye YouTube na Facebook.
 
Akiwa ameshika Biblia mkono wake wa kulia katika bustani ya jijini Nairobi, Odinga alitangaza kuwa anajibu "wito wa ngazi ya juu kuchukua ofisi ya rais wa watu wa Jamhuri ya Kenya."
 
Watu wamechoshwa na wizi wa kura katika uchaguzi na tukio hilo lilikuwa hatua kuelekea ujenzi wa demokrasia sahihi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki, Odinga aliuambia umati uliokuwa ukishangilia.
 
Aliyekuwa mgombea mwenza wake, Kalonzo Musyoka, hakuwapo kwenye hafla hiyo. Odinga alisema ataapishwa siku nyingine.
 
Akizungumza awali na televisheni ya Kenya ya KTN, Odinga alisema kufungwa kwa vyombo vya habari "kumethibitisha kuwa tumeporomoka kufikia kiwango cha Uganda", ambayo ilisimamisha matangazo ya vyombo vya habari wakati wa uchaguzi mwaka 2016.
 
"Kuapishwa kwake" kulikuwa na lengo la "kuonyesha dunia kuwa tunachofanya ni halali kisheria, kikatiba na kitu ambacho huwezi kukielezea hata kidogo kuwa mapinduzi", alisema zaidi.
 
Vituo vitatu binafsi vya televisheni - NTV, KTN na Citizen TV - vilizima matangazo kuanzia saa 3:10 asubuhi.
 
Citizen TV iliiambia BBC kuwa mamlaka za serikali ziliwalazimisha kuzima matangazo kutokana na mipango ya kuonyesha mkusanyiko huo.
 
Watazamaji wa KTN walishuhudia vioo vya luninga zao vikishika rangi nyeusi wakati mtangazaji akisoma taarifa kutihibitisha kuwa mamlaka ya mawasiliano ilikuwa ikizima matangazo.
 
Kuzimwa kwa 'signo' ya matangazo ya vyombo vya habari si jambo la kawaida hapa Kenya.
 
Palikuwa na wasiwasi jana huku baadhi ya shule katika mji mkuu wa Kenya zikifungwa kwa sababu ya tukio hilo, na watu kutojua nini kingetokea.
 
Polisi awali walizingira viwanja hivyo, lakini baadaye wakaondoka.
 
BBC
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment