Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amezungumzia hali ya afya yake akisema kwa sasa anachoweza kukifanya ni kusimama peke yake na ili atembee anahitaji msaada wa magongo.
Lissu ambaye pia ni rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS) anayeendelea na matibabu ya viungo katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven nchini Ubelgiji alisema hayo jana alipozungumza na Mwananchi.
“Mie naendelea vizuri na kwa sasa ninaweza kusimama kidogo tu. Sijaanza kutembea bila magongo,” alisema.
Kuhusu hali ya mguu wa kulia ambao uliathirika zaidi na risasi alizoshambuliwa Septemba 7, 2017 mjini Dodoma, alisema: “Bado sio salama sana na unahitaji kufanyiwa kazi ya kitabibu zaidi.”
Awali, Lissu kupitia ukurasa wake wa mtandao wa jamii wa Instagram aliandika ujumbe wa kumshukuru Mbunge wa Tandahimba (CUF), Ahmad Katani aliyemtembelea Ubelgiji na picha ya wawili hao ilianza kusambaa juzi usiku mitandaoni ikiwaonyeasha wakiwa na nyuso za furaha.
Lissu alimshukuru mbunge huyo kwa kumtembelea huku akieleza kuwa ni miongoni mwa wabunge waliompeleka Nairobi nchini Kenya akitokea Hospitali ya Rufaa ya Dodoma alipopelekwa baada ya kushambuliwa.
“Katani alikuwa kwenye msafara wa wabunge walionipeleka Nairobi, Kenya mara baada ya jaribio la mauaji la Septemba 7 na alikaa Nairobi kwa siku nne. Nimefarijika sana na ugeni huu wa ndugu yangu na kaka yangu Katani,” alisema mbunge huyo.
0 comments :
Post a Comment