Rais Magufuli Kawapa Siku 7 Mawaziri Wake

Rais Dkt. John Magufuli ametoa wiki moja kwa Mawaziri kufanyia kazi changamoto na maoni yaliyotolewa na wafanyabiashara katika mkutano wa 11 wa Baraza la Taifa la Biashara ili kuweza kutatua kero zao.

Amewataka Mawaziri kuandika maelezo yenye majibu ya changamoto na maoni hayo na kuwasilisha kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ili serikali ifanyie kazi na kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini.

Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa baraza hilo ametoa maagizo hayo jana wakati akihitimisha mkutano huo ambao wafanyabiashara na wawekezaji kutoka sekta mbalimbali walipata nafasi ya kueleza maendeleo ya shughuli zao, changamoto zinazowakabili na mapendekezo ya kuimarisha biashara na uwekezaji hapa nchini.

Miongoni mwa changamoto zilizoweza kuwasilishwa katika mkutano huo ni pamoja na utozaji wa kodi unaoathiri biashara na uwekezaji, urasimu wa taasisi za serikali, udhibiti wa bidhaa za kutoka nje ya nchi zinazoathiri uzalishaji wa bidhaa za ndani, uwepo wa sheria na kanuni kandamizi kwa biashara na uwekezaji na utendaji usioridhisha kwa baadhi ya maafisa wa Serikali.

“Nataka kuwaambia kwa dhati kabisa, serikali ninayoiongoza haiwachukii wafanyabiashara, inawapenda na itawaunga mkono, kama nilivyowaambia huko nyuma huu ndio wakati wenu wa kufanya biashara, fanyeni biashara zenu na lipeni kodi, hizi changamoto tumezipokea na tutazifanyia kazi”, alisema Dkt. Magufuli.

Kwa upande mwingine, Rais Magufuli ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kuhakikisha wanashiriki katika miradi mikubwa anayotekelezwa na serikali ikiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge), mradi wa umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima – Uganda hadi bandari ya Tanga – Tanzania, na amewataka wafanyabiashara wanaofanya vitendo vya udanganyifu katika kodi na uingizaji wa bidhaa wabadilike.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment