Rais Magufuli ameendelea kusisitiza kuwa hatobadilika na ataendelea kuwa yule yule katika kuwatumikia wananchi.
Pia amesema serikali itamega maeneo ya ardhi ya hifadhi na kuwapa wananchi ili yatumike katika shughuli za maendeleo.
Ametoa msimamo huo leo alipokuwa akifungua matumizi ya barabara ya Uyovu- Bwanga km 45 katika eneo la uyovu runzewe wilayani Bukombe mkoani Geita.
“Sitobadilika kamwe mimi ni yule yule nitaendelea kuwatumikia watanzania wote,’’ amesema Magufuli
Kuhusu ardhi amesema hatua ya kumega ardhi ya hifadhi ni kufuatia kuwepo kwa ongezeko la idadi ya watanzania tangu nchi kupata uhuru.
“Ni ukweli usiopingika ni lazima maeneo ya hifadhi yamegwe na kupewa wananchi kwa ajili ya shughuli za maendeleo hii ni kutokana na kwamba idadi ya watanzania imeongeza maradufu tangu nchi ipate uhuru,’’ amesema Magufuli
Amewata wananchi kuwa na subra na kwamba serikali ipo katika mchakato wa kutoa maeneo hayo.
Rais amesema kutokana na ongezeko la watu maeneo ya kulima na ufugaji yamepungua kwa kiasi kikubwa.
Akitolea mfano amesema kwa sasa matumizi ya ardhi kwa wilaya ya Bukombe ni asilimia 40 na asilimia 60 ni hifadhi.
“Hakuna sababu ya kuandamana wala kupigana kugombea ardhi, serikali itatoa ardhi,’’ alisisitiza.
Barabara hiyo ni kiunganishi cha mikoa ya Geita, Shinyanga, Kigoma, Kagera pamoja na nchi ya Rwanda
0 comments :
Post a Comment