Tanzania na Israel zimekubaliana kwamba , mataifa hayo mawili yana mengi ya kujifunza baina yao hususani katika eneo la utoaji wa haki na usimamiaji wa sheria.
Hayo yamejiri jana ( jumatatu) wakati Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi, alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Sheria wa Israel Bi. Ayalet Shaked.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika katika Jengo la Mikutano la Kimataifa la Mwalimu Julius Nyerere ( JNICC), viongozi hao walikubaliana kwamba kuna haja na umuhimu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Israel kukutana kwa lengo la kuainisha maeneo ambayo Ofisi hizo mbili zinaweza kushirikiana.
“ Nadhani tuna mengi ya kujifunza kutoka kwenu na halikadhalika nanyi kuna maeneo ambayo mnaweza kujifunza kutoka kwetu. Hivyo basi, ninaamini kwamba pale itakapowezekana, kuna umuhimu wa mimi kukutana na mwenzangu ili tuweze kuangalia maeneo ya kipaumbele ambayo tunaweza kubadilishana uzoefu na kupanua wigo wa ushirikiano baina ya nchi zetu”, akasema Dk. Kilangi.
Akayataja maeneo ambayo anaamini Tanzania na Israel zinaweza kushirikiana ni pamoja na namna bora ya kuimarisha mifumo ya utoaji haki na ushauri wa kisheria wenye tija, pamoja na eneo la uwezeshwji ( capacity building).
Mwanasheria Mkuu , Dk. Kilangi ambaye alifuatana na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw, Edson Athnas Makallo, aliyatumia mazungumzo kati yake na Waziri Shaked kuelezea baadhi ya majukumu yake anayoyatekeleza kama Mshauri Mkuu wa Serikali katika masuala yote yanayohusu sheria pamoja muundo mpya wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ambao umehusisha kuanzishwa kwa Wakili Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Waziri wa Sheria wa Israel, ambaye Tanzania inakuwa nchi yake ya kwanza kutembelea Barani Afrika, pamoja na kukubaliana na wazo la Dk. Kilangi la kuangalia uwezekano wa Wanasheria Wakuu kukutana katika muda utakaopangwa. Amesema kwamba, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ni Ofisi nyeti na yenye hadhi ya juu kabisa katika nchi yoyote ile ikiwamo Israel.
Akaongeza kwamba, majukumu anayoyatekeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk. Adelardus Kilangi yanashabihiana na anayotekeleza Mwanasheria Mkuu wa Israel yakiwamo ya kuisimamia serikali katika masuala yote yanayohusu sheria, kuiwakilisha serikali katika mahakama za juu na mahakama za chini pamoja na kuendesha mashauri ya jinai hivyo wawili hao wakipata fursa ya kukutana bila shaka watakuwa na mengi ya kujadiliana na kushirikiana.
Waziri wa Sheria wa Israel Ayalet Shaked anaongoza ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Israel ambao upo hapa nchini kukutana na wafanyabiashara wa Tanzania
0 comments :
Post a Comment