Waziri wa Nchi Ofisi anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amemuagiza Msajili wa vyama vya Siasa kuchukua hatua kwa vyama vinavyokiuka sheria na miongozo ya vyama vya siasa.
Ametoa kauli hiyo jana (Aprili 23, 2018) alipokuwa akitoa maelezo ya ufafanuzi juu ya hoja za ofisi yake, zilizoainishwa katika Ripoti ya Mthibiti na Ukaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa Mwaka wa fedha unoishia Juni 30, 2018 alipokutana na waandishi wa habari Bungeni Dodoma.
Waziri Mhagama ameelekeza kuhakikisha vyama vyenye mapungufu upande wa hesabu zao basi wawasilishe kwa Msajili wa vyama ndani ya wiki 3 hadi 4.
“Namtaka Msajili wa Vyama achukue hatua za Kisheria pasi kusita kwa chama chochote kinachokiuka sheria ya vyama vya siasa Na. 2 ya mwaka 1992”.alisema Waziri Mhagama
Aidha amemtaka Msajili wa Vyama vya siasa nchini kuhakikisha anaweka miongozo na mpango kazi ili vyama vilivyozoea kutowasilisha hesabu zao viache mara moja kwa mujibu wa sheria.
Waziri Mhagama aliongezea kuwa taarifa ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ilibaini mapungufu kadhaa katika uendeshaji wa vyama vya siasa ikiwemo; Upungufu katika hesabu zilizowasilishwa chini ya viwango vya Kimataifa vya uandaaji wa hesabu katika sekta za umma na baadhi ya vyama kushindwa kuwasilisha hesabu zao kwa CAG kwa ukaguzi
Pamoja na hayo alibainisha kuwepo kwa vyama vya kisiasa visivyotumia rejista ya mali za kudumu ambapo vyama vinne ikiwemo;CHADEMA, NLD,ADC na Demokrasia Makini havina Daftari la kudumu la mali zao ikiwa ni kinyume na sheria zilizopo.
“Msajili wa Vyama nakuagiza kutoa maelekezo kwa kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu kuwa na regista ya mali zake ndani ya wiki tatu kuanzia leo kwani kukosa daftari la mali za kudumu ni kinyume na kifungu Na.14(1)(b)(ii) ya sheria ya vyama vya siasa Na.5 ya mwaka 1992.”alisisitiza Waziri.
Sambamba na hilo Waziri alimtaka Msajili wa Vyama vya siasa kuhakikisha vyama vyote vinafuata miongozo yote ya kihasibu ili kuondokana na mapungufu ya kukosekana kwa nyaraka za malipo kama ilivyobainishwa na mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali ambapo alibaini vyama vitatu kati ya tisa vina nyaraka pungufu ikiwemo CHADEMA, SAU na ADC.
“Msajili wa vyama ahakikishe vyama vya siasa vinatekeleza miongozo yote kihasibu pamoja na kanuni za fedha, ambazo zinaelekeza nyaraka ziwe na viambatisho sahihi kwani ripoti ilibainisha vyama vitatu vilikuwa na malipo yenye nyaraka pungufu zenye thamani ya shilingi 735,978,559 ambapo ni kinyume na miongozo ya kihasibu na kukosa uhalali wa malipo hayo.”alisisitiza Waziri Mhagama.
Awali kifungu cha 14(1)(a) na (b)(i) cha Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258 [RE: 2015] kinaelekeza kuwa, kila chama cha siasa kinapaswa kutunza taarifa za mapato na matumizi, ikiwamo taarifa za mali zake. Vile vile, kinapaswa kuwasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Siasa, taarifa ya hesabu zake zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), pamoja taarifa ya mali zake.
Hivyo, Kifungu hicho kinampa mamlaka Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kufanya ukaguzi wa hesabu za kila chama cha siasa chenye usajili wa kudumu. Katika mwaka wa fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2017, CAG amefanya ukaguzi wa hesabu za Vyama vya Siasa kumi ikiwemo; CCM, CHADEMA, NLD, TLP, Demokrasia Makini (MAKINI), TLP, DP, SAU, AFP, CCK na ADC kati ya vyama vya siasa kumi na tisa vyenye usajili wa kudumu. Vyama vya Siasa tisa (9) havikuwasilisha hesabu zake kwake kwa wakati kwa ajili ya ukaguzi, hivyo hakukaguliwa
0 comments :
Post a Comment