Wanamgambo wa Kipalestina huko Gaza wamevurumisha makombora kadhaa kusini mwa Israel jana. Hata hivyo mashambulizi hayo hayakusababisha majeraha, lakini yameongeza hali ya wasiwasi katika eneo la mpakani.
Taarifa ya jeshi la Israel ilisema makombora 25 yamevurumishwa kuelekea maeneo kadhaa nchini Israel, huku mengi yakizuiwa na mfumo wa kuzuia makombora wa Iron Dome. Polisi walisema makombora kadhaa yameanguka katika maeneo ya wazi upande wa Israel, lakini hakuna ripoti zozote za majeruhi zilizotolewa.
Jeshi lilisema makombora mengine mawili yalifyatuliwa kutokea Gaza baada ya mfululizo wa kwanza wa makombora, moja limelipuka karibu na jengo la shule ya chekechea lakini inaaminiwa hakukuwa na mtoto yeyote ndani ya jengo hilo wakati wa tukio.
Duru za usalama za Palestina zilisema vifaru vya Israel vimeyashambulia maeneo ya kufuatilia matukio ya makundi ya Hamas na Islamic Jihad karibu na mpakani. Msemaji wa jeshi la Israel alisema hana taarifa kuhusu hujuma hiyo.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, aliapa kuchukua hatua kali. "Israel huchukulia kwa uzito mkubwa mashambulizi dhidi yake na jamii zake yanayofanywa na Hamas na Islamic Jihad kutokea Ukanda wa Gaza. Jeshi la Israel litajibu mashambulizi haya kwa nguvu," alisema Netanyahu wakati wa mkutano kaskazini mwa Israel.
0 comments :
Post a Comment