Watu 2 wamefikishwa Mahakama ya hakimu mkazi Mkoa Tabora kwa kosa la kuhujumu uchumi.
Watuhumiwa hao waliofikishwa mahakamani jana kwa kosa la kung'oa miundombinu ya barabara ni Mohamed Abdallah na mwanae Ramadhan Mohamed.
Wakili wa Serikali ,Innocent Rweyemamnu, aliiambia mahakama mbele ya hakimu Judica Nkya, aliyeisikiliza kwa niaba ya hakimu mkazi, Joctan Rushwela, kuwa washitakiwa waliharibu miundombinu ya barabara yenye thamani ya Shilingi milioni62.
Ameieleza mahakama kuwa washitakiwa walifanya uharibifu huo katika kijiji cha Upungu kilichopo wilayani Nzega tarehe 9 mwezi uliopita.
Washitakiwa katika Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 13/2018 hawakutakiwa kujibu chochote na kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 18 mwezi huu itakapotajwa tena na mahakama.
Miundombinu iliyoharibiwa ni vyuma ambavyo vinatumika kama kingo za kuzuia ajali za magari yanayo hama barabarani na kupunguza madhara kwa gari linapopata ajali na hivyo kuokoa mali na abiria wanaokuwepo ndani yake.
Vyuma vilivyong’olewa ni kwenye maeneo ya wilaya za Uyui na Nzega katika barabara Kuu ya Tabora hadi Nzega iliyozinduliwa na Rais John Magufuli mwezi wa nane mwaka jana.
0 comments :
Post a Comment