Rais Magufuli Kuzindua Programu Ya Kuendeleza Sekta Ya Kilimo Awamu Ya Pili (ASDP II)

Na Mathias Canal-WK, Dar es salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uzinduzi wa programu ya kuendeleza sekta ya kilimo awamu ya pili (ASDP II) tarehe 4 June 2018.

Katika dhifa hiyo inayotarajiwa kuanzia Saa 2.00 asubuhi katika jengo la Mikutano la kimataifa la Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam, Rais Magufuli ataambatana na wageni wengine wa kitaifa na kimataifa akiwemo makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa, Mkuu wa Mkoa wa Dara es salaam Mhe Paul Makonda, Mawaziri wa sekta za kilimo pamoja na wadau wote wa sekta ya hiyo.

Taarifa ya uzinduzi wa Programu hiyo ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini imetolewa jana 1 June 2018 na waziri wa kilimo Mhe Dkt. Charles Tizeba wakati akizungumza na waandishi wa habari katika jengo la Mikutano la kimataifa la Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es salaam.

Dkt Tizeba alisema, Wizara za kisekta zikijumuisha Wizara ya Kilimo, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za mitaa-TAMISEMI, Wizara ya Viwanda Biashara na Uwekezaji, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maji na Umwagiliaji  ndizo zenye jukumu la kuhakikisha ASDP II inakuwa na mafanikio makubwa nchini na kuwa mkombozi wa wananchi katika kilimo.

Alisema kuwa ASDP II itatekelezwa katika mikoa na wilaya zote kwa kuzingatia mazao ya kipaumbele kufuatana na ikolojia ya kilimo ya kanda kwa miaka kumi (10) kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano ambapo kipindi cha kwanza kitaanza 2018/19 hadi 2023/24.

Katika hatua nyingine Dkt Tizeba ametaja lengo la Programu hiyo kuwa ni kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo ili kuongeza uzalishaji na tija  katika kilimo, mifugo na uvuvi; kuongeza pato la wakulima, wafugaji na wavuvi; kuongeza pato la Taifa na kuwa na uhakika wa usalama wa chakula na lishe.

Aidha, Programu hii itatekeleza sera mbalimbali kama vile Sera ya Kilimo ya Taifa, Sera ya Mifugo ya Taifa, Sera ya Uvuvi, Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo, Sera ya Umwagiliaji ya Taifa, Sera ya Usalama wa Chakula na Lishe, Sera ya Ugatuaji Madaraka, Sera ya Maendeleo ya Ushirika na Sera ya Mashirikiano kati ya Sekta za Umma na Sekta Binafsi.

Katika hatua nyingine Mhe Dkt Tizeba ameuarifu umma wa watanzania kuwa endapo mpango huo utatekelezwa kama ilivyopangwa hadi kufikia mwaka 2022 Tanzania itakuwa katika uchumi wa kati.

Katika utekelezaji wa ASDP II washiriki ni wadau wa sekta ya Kilimo, Mifugo, Uvuvi, Ushirika, Wizara, Taasisi za Serikali na zisizo za Serikali, Washirika wa Maendeleo, Sekta Binafsi na wananchi wote.

MWISHO.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment