Polisi akilinda Kituo cha Kupigia Kura cha Shule ya Chekechea ya
Mchwivila katika Jimbo la Kalenga, Iringa jana . Picha na Edwin
Mjwahuzi
Na Mwananchi
Kwa ufupi
Katika tukio linalopaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na
wapenda amani wote pasipo kujali misimamo yao ya kisiasa, walinzi wa
kikosi hicho walimteka, kumtesa na kumdhalilisha mbunge wa Viti Maalumu,
Rose Kamili wa Chadema ndani ya ofisi za CCM mkoani Iringa kwa madai ya
kumkuta akitoa rushwa, huku yeye akisema alikuwa akitoa maelekezo kwa
mawakala wa chama chake.
Uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Kalenga,
mkoani Iringa ulimalizika mwishoni mwa wiki na Chama cha Mapinduzi
(CCM), kiliibuka mshindi. Uchaguzi huo ulikuwa wa kuziba nafasi
iliyoachwa wazi na Dk. William Mgimwa aliyefariki dunia Januari mwaka
huu. Tunaipongeza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa kuendesha uchaguzi
ulio huru na haki. Pamoja na kujitokeza kasoro ndogondogo za hapa na
pale, tume hiyo ilisimamia na kuendesha uchaguzi huo kikamilifu na kutoa
haki kwa vyama vilivyoshiriki pasipo kupindisha sheria.
Huu ni utamaduni mpya katika nchi yetu, kwani sote
ni mashahidi wa jinsi chaguzi mbalimbali zilizofanyika huko nyuma
zilivyokuwa zikiendeshwa kwa mizengwe. NEC ilikuwa ikikiuka waziwazi
kanuni na sheria za uchaguzi, hasa kutokana na shinikizo kutoka kwa
wanasiasa na baadhi ya viongozi serikalini. Vyombo vya ulinzi na usalama
navyo vilichangia kuwapo kwa kasoro nyingi katika chaguzi hizo kutokana
na kuegemea upande mmoja na kukandamiza upande wa pili.
Wakati tukiipongeza Tume hiyo kwa kuendesha na
kusimamia uchaguzi huo vizuri, hatuna budi kulaani vitendo vya kihuni na
kiharamia vilivyofanywa na kikosi cha ulinzi cha CCM kinachojulikana
kama Green Guards. Katika tukio linalopaswa kulaaniwa kwa nguvu zote na
wapenda amani wote pasipo kujali misimamo yao ya kisiasa, walinzi wa
kikosi hicho walimteka, kumtesa na kumdhalilisha mbunge wa Viti Maalumu,
Rose Kamili wa Chadema ndani ya ofisi za CCM mkoani Iringa kwa madai ya
kumkuta akitoa rushwa, huku yeye akisema alikuwa akitoa maelekezo kwa
mawakala wa chama chake.
Mbunge huyo sasa amelazwa katika Hospitali ya
Rufaa ya Mkoa wa Iringa. Katika tukio hilo, polisi wanadaiwa kumgeuzia
kibao na kumfungulia mashtaka badala ya kuwakamata makada hao wa CCM
waliomteka na kumtesa kwa tuhuma za kutunga. Pia katika tukio la awali,
walinzi hao wanadaiwa kumteka na kumtesa padre wa Kanisa la Orthodox
katika Parokia ya Nyamihu, Costantino Mbilinyi kwa kumhusisha na kampeni
za moja ya vyama vya siasa vilivyokuwa vikishiriki katika
kinyang’anyiro hicho.
Hakuna asiyejua kwamba kujichukulia sheria mkononi
ni kosa la jinai. Jukumu la kila mwananchi ni kutoa ripoti polisi au
katika vyombo vingine vya ulinzi na usalama pale anapomwona mtu yeyote
akitenda kosa. Kama walinzi wa kikosi cha Green Guards cha CCM walimkuta
mbunge huyo akitoa rushwa walipaswa kutoa ripoti polisi na kutoa
ushahidi badala ya kumteka, kumpeleka katika ofisi za chama hicho
kumtesa na kumdhalilisha. Kama kweli walikuwa na nia njema, kwa nini
walishindwa kutoa ripoti Takukuru ambacho ndicho hasa chombo
kinachohusika na kupambana na vitendo vya rushwa?
Tumekuwa tukisema kwamba vikosi vya ulinzi vya
baadhi ya vyama vya siasa vya Green Guards, Blue Guards na Red Brigades
vinafanya vitendo vya jinai, hivyo vipigwe marufuku ili kuinusuru nchi
yetu na vita au balaa zozote zinazoweza kuchochewa na vikosi hivyo.
Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anasema anatafuta dawa
ya kukomesha vurugu zinazojitokeza mara kwa mara katika chaguzi
zinazofanyika sehemu mbalimbali nchini. Hilo ni wazo jema. Tunamshauri
aanze kwa kupiga marufuku vikosi hivyo vya mgambo vya vyama vya siasa
ili makosa yaliyojitokeza Kalenga yasijirudie katika uchaguzi wa Jimbo
la Chalinze utakaofanyika mwezi ujao.
0 comments :
Post a Comment