Kwa ufupi
Ukweli ni kuwa ndani ya nchi yao Watanzania hawana
raha. Kila siku ni mateso kutoka kwa wale tuliowatarajia kuwa huenda
wangekuwa watetezi wao.
Katika baadhi ya maeneo nchini, wananchi
wananyang’anywa ardhi zao kwa nguvu ili kupisha wawekezaji wa kigeni
watumie ardhi hiyo.
Iko haja ya kuwapasulia ukweli viongozi wetu. Hata
kama mmeamua kutunyonya wananchi na kuchota asali na maziwa yote ya
nchi, basi msile na kutapanya rasilimali zote. Vizazi vyenu na vyetu
vitakuja kula nini?
Madini sasa yanatoweka, ardhi yenye rutuba nzuri
mmejimilikisha ekari zake kwa maelfu, achilia mbali mnazowanyanganya
wananchi kila siku kwa kisingizio cha uwekezaji au kulinda maeneo ya
hifadhi.
Sasa mnanuwia kuwapa wageni gesi na mafuta, huku
mkiwatenga na kuwaponda wazawa. Hivi nchi hii itabakiwa na nini miaka
100 ijayo?
Kama waasisi wa Taifa hili wangetapanya rasilimali
enzi zao, leo mngepata kiburi cha kuwasimanga wazawa kuwa hawana uwezo
wa kuwekeza katika sekta za gesi na mafuta?
Sisi wananchi hatuna shida na kula kwenu. Kuleni
na msaze lakini wekeni mazingira mazuri ya kila Mtanzania kuishi japo
maisha ya kawaida. Jengeni barabara ili mkipita na mashangingi yenu,
sisi tupite na baiskeli au pikipiki zetu.
Iko wapi raha ya kuendesha gari la Sh200 milioni
katika barabara yenye viraka na mashimo? Tuwekeeni miundombinu ya maji
na umeme, ili hata msipolipa bili, sisi wanyonge tutawafidia kwa
kulipishwa bei kubwa, ili Tanesco iweze kujiendesha.
Simamieni kikamilifu mifumo ya kodi ili watu wengi
zaidi wakiwamo wafanyabiashara, wapangishaji wa nyumba na fremu nao
walipe kodi badala ya kutegemea kodi za wafanyakazi pekee. Kodi ikiwa
kubwa hamuoni kuwa nanyi mtapata fungu kubwa zaidi la kulipana
mishahara, posho na kufanya ‘’matanuzi’?
Mnapojiita viongozi kwa maana ya uwaziri, umeya,
ukuu wa mkoa, ukurugenzi wa halmashauri na vyeo vingine, hamuongozi miti
na mawe, mnawaongoza watu waitwao Watanzania.
Hawa ndiyo wanaowafanya nyinyi mkaitwa viongozi na
hatimaye kutambulika ndani na nje ya nchi. Hata kula kwenu kunatokana
na wao, kwani ndiyo wanaohenyeka ili nyinyi wakubwa mtembelee
mashangingi na kuishi katika majumba ya kifahari jirani na fukwe za
bahari.
0 comments :
Post a Comment