Spika wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta akitoa ufafanuzi jinsi
kamati za kudajili vifungu vya Rasimu ya Katiba zitakavyokuwa zinafanya
kazi, kabla ya kuahirisha Bunge mjini Dodoma jana. Picha na Salim Shao
Kwa ufupi
Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba, Mchungaji
Christopher Mtikila amedai hataweza kuchangia tena katika mjadala wa
Katiba kwa kuwa Ofisi ya Bunge imempiga marufuku kutokana na kauli zake.
Hata hivyo, Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba,
Yahaya Khamis Hamad alisema kuwa taarifa hiyo kwake ni mpya na haamini
kuwa jambo hilo lipo.
“Hili kwangu ni jipya na sidhani kuwa linawezekana na lipo,” alisema Hamad.
Awali Mtikila aliliambia gazeti hili kuwa amepewa
barua hiyo Jumatano iliyopita, ikiwa ni majibu ya barua yake
aliyoandikia ofisi hiyo ya Bunge kutaka ufafanuzi wa kile alichoeleza
kuwa amekuwa akinyimwa haki ya kuchangia bungeni.
“Nilianza kuhisi baada ya kuona kuwa nanyimwa
kuchangia, nikaandika barua kuomba maelezo kwa nini ninakosa nafasi ya
kuchangia bungeni,” alisema Mtikila na kuongeza;
“Lakini juzi nilipokea barua kutoka kwa Katibu wa
Bunge ikinikataza kuchangia tena bungeni kutokana na statement (taarifa)
zangu za kukosewa kwa mchakato.”
Alisema kuwa alipomuuliza katibu kulikoni akatazwe
kuchangia katika Bunge hilo alijibiwa kuwa ni maagizo kutoka kwa
mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta.
Mchungaji Mtikila alisema kutokana na katazo hilo atamwona Sitta ili amfafanulie tatizo lake.
“Hii imeniathiri sana mimi. Bunge hili limepotoka wanachoangalia ni masilahi yao na si ya nchi,” alisema.
Alisema mchakato wote umekosewa kwa kuwaweka
wabunge na wawakilishi kuwa sehemu ya Bunge badala ya wananchi kuchagua
wajumbe wa Bunge hilo.
“Hakuna nchi yoyote ambayo imefanya hivyo,
wanaharibu mabilioni ya fedha ambayo hayataleta Katiba yenye uhalali
yoyote,” alisema.
Alisema endapo Sitta atashindwa kutatua jambo hilo
anakusudia kuunganisha katika ushahidi wake kwenye kesi inayopinga
mchakato wa Katiba.
0 comments :
Post a Comment