Mjumbe wa Bunge la Katiba wa kundi la Umoja wa Kutetea Katiba ya
Wananchi (Ukawa), Ismail Jussa akionyesha moja ya nukuu za kitabu cha
Profesa Issa Shivji wakati wa mkutano na waandishi Dodoma jana. Kushoto
ni mjumbe mwenzake, Tundu Lissu. Picha na Salima Shao
Na Waandishi Wetu, Mwananchi
Kwa ufupi
Akizungumzia hotuba hiyo, Jussa aliyeweka wazi
masilahi yake kuwa ni mwanafunzi wa Profesa Shivji, alisema msomi huyo
aliyekuwa tegemeo la wanyonge, alifanya upotoshaji mkubwa ambao umetoa
vitisho kwa wananchi.
Dar /Dodoma/Mwanza. Ni dhahiri
kwamba mjadala wa msomi wa Sheria, Profesa Issa Shivji umewavuruga
wanasiasa waumini wa serikali mbili ambao baadhi yao jana walimshukia
wakidai kuwa “mzee huyu ni ndumila kuwili na kigeugeu.”
Shivji juzi alitoa mjadala kuhusu muundo wa
Muungano na kuishutumu Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopendekeza
serikali tatu, kuwa ilipotosha maoni ya wananchi. Alipotakiwa
kuzungumzia madai dhidi yake, Profesa Shivji alisema: “Nyie ni waandishi
wa habari someni, angalieni wapi mimi nilisema Serikali tatu, wanaosema
ninatumiwa na CCM hayo ni maoni yao siwakatazi kuzungumza
wanachofikiria.”
Jana Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) katika
kampeni yake nje ya Bunge la Katiba, ulimtaka Profesa Shivji kuwaomba
radhi wananchi kwa kile wanachodai kwamba amekuwa kigeugeu kwenye
maandishi na matamshi yake kuhusu muundo wa Muungano.
Katika mkutano wake wa kuelimisha wananchi kuhusu
Katiba Mpya mjini Mwanza uliojaa polisi kila kona, Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk. Willibrod Slaa alisema wanamshangaa Profesa Shivji kwa
mawazo yake yasiyoeleweka kuhusu muundo wa Muungano.
“Kwa kweli tunaamini watu ambao ni wasomi kama
Profesa Shivji wanaweza kuwasaidia wananchi kupata katiba nzuri, lakini
anachokifanya sasa ni siasa, jambo ambalo siyo jema,” alisema Dk. Slaa
na kuongeza:
“Ukawa tunamtaka awaombe radhi wananchi, kwani
amewadhalilisha kwa kuwa kigeugeu. Mara ya kwanza tunakumbuka alikuwa
muumini wa Serikali tatu leo anageuka na kuanza kuhubiri serikali mbili,
huu ni upuuzi kwa msomi kama yeye kufanya hivyo.”
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe alisema CCM wanaogopa Rasimu ya Katiba kwa sababu wamezoea uchakachuaji.
Naye Kaimu Katibu Mkuu wa CUF, Abdulkarim Kambaya
alisema Rais Kikwete amewachezea akili wananchi, kwani awali alikuwa
anaonyesha yupo upande wao lakini kupitia hotuba yake bungeni amewakana
na kuibeba CCM.
Lissu, Jussa nao wanena
Pia baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba wanaounda
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walimshambulia kwa maneno
Profesa Isa Shivji kuwa ni ‘ndumilakuwili’.
Kwa nyakati tofauti, wajumbe Tundu Lissu na Ismail
Jussa walisema kuwa Profesa Shivji “alibebwa na CCM na kulishwa maneno
kwa masilahi ambayo hayajulikani.”
Akizungumzia hotuba hiyo, Jussa aliyeweka wazi
masilahi yake kuwa ni mwanafunzi wa Profesa Shivji, alisema msomi huyo
aliyekuwa tegemeo la wanyonge, alifanya upotoshaji mkubwa ambao umetoa
vitisho kwa wananchi.
0 comments :
Post a Comment