Sunday, June 28, 2015
Nkupamah blog
CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kina shabaha ya kurejesha kwa wananchi mashamba ya mkonge yaliyouzwa kwa matajiri wachache ambao kwa sasa hawayatumii kwa kilimo cha zao hilo.
Pia chama hicho kimeazimia kurejesha Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) wa Watanzania ili nchi iweze kujitegemea kiuchumi.
Kauli
hiyo imetolewa juzi na Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe akiwa
jijini Tanga alipokuwa akikitambulisha chama hicho kipya kwa wananchi.
“Mwaka
2014 mkonge umechangia dola za Marekani milioni 16 katika mauzo ya
bidhaa nje, hiki ni kiwango kidogo mno, mashamba yapo lakini yameuzwa
kwa matajiri wachache na hayazalishi.
“Chama
chetu kinataka mashamba haya waliyouziwa matajiri ambayo hayazalishi
wapewe wananchi, Azimio la Tabora limetamka hilo kinaga ubaga,” alisema Zitto.
Alisema
ardhi na mashamba yote yaliyokuwa ya mashirika ya umma na kubinafsishwa
yarejeshwe kwa wananchi wasio na ardhi kwa kuwagawia na kushiriki
katika uzalishaji kwa kutumia mfumo wa ‘out growers scheme’.
Zitto
alisema mashamba makubwa ya kibiashara yatakapohitajika itakuwa ni
jumla ya mashamba madogo madogo ya wananchi na pale uwekezaji
utakapohitaji basi wananchi watamiliki theluthi mbili ya shamba husika
na mwekezaji wa ndani au wa nje atamiliki theluthi moja tu.
“Tunataka mkonge ulimwe na wakulima wadogo ili Watanzania wawe na shughuli za kilimo zenye tija,” alisema.
Akizungumzia
mabenki, alisema Azimio la Tabora limeagiza dola kumiliki benki kubwa
nchini ili kujitegemea kiuchumi kwani nchi haiwezi kuendelea iwapo
mabenki makubwa yote yanamilikiwa na watu kutoka nje.
Zitto
alisema malengo ya kujenga uchumi shirikishi wenye uhuru mkubwa katika
soko la mitaji hayawezi kufikiwa bila ya kuwa na benki zinazomilikiwa na
Watanzania wenyewe.
Alisema
ACT-Wazalendo itahimiza Benki ya Taifa ya Biashara irejeshwe kwenye
mikono ya Watanzania kwa kumilikiwa na Serikali kwa asilimia 50 na
wananchi na taasisi za wananchi kupitia soko la mitaji nusu iliyobakia.
Zitto alisema chama chao kitahimiza pia Benki ya Maendeleo na Benki ya Kilimo kuwa na muundo wa umiliki kama wa NBC.
Kiongozi
huyo alisema ubinafsishaji wa NBC ulifanywa holela na benki iliuzwa kwa
bei ya bure, na kwamba msimamo huo wa chama chao unaungwa mkono na kazi
iliyofanywa na Kamati ya Bunge ya PAC iliyoagiza ukaguzi maalumu kwenye
mchakato wa ubinafsishaji huo.
“Tunataka
kurejesha nafasi ya Tanga kwenye taifa letu. Tunaomba muunge mkono
chama chetu, tunawakabidhi chama hiki watu wa Tanga, ni chama chenu na
kiwe jukwaa lenu katika kupaza sauti za wanyonge.
“Tanga
ni mkoa uliokuwa mstari wa mbele katika kulikomboa taifa letu. Chama
cha TANU kilisheheni viongozi kutoka Tanga. Kina Stephen Muhando na
Mwalimu Kihere kwa nyakati tofauti walikuwa watendaji wakuu wa TANU
wakati tunasaka uhuru wa nchi yetu,” alisema.
Zitto
alisema Tanga bado ina nafasi kwenye uchumi wa nchi, inashika nafasi ya
8 katika mchango kwa pato la taifa, unashika nafasi ya 3 katika
makusanyo ya kodi nchini baada ya Dar es Salaam na Arusha.
Nkupamah blog
0 comments :
Post a Comment