Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana
akizungumza katika mkutano wa hadhara kwenye viwanja vya furahisha
jijini Mwanza jana.Picha na Michael Jamson.
Akihutubia katika mkutano wa kuhitimisha ziara yake, jijini Mwanza jana,
Kinana alisema atafanya kikao cha kwanza na wabunge wa CCM baada ya
uchaguzi ili kuwaeleza majukumu yao ya msingi ikiwamo kuiwajibisha
Serikali.
Alisema wabunge wa CCM wamekuwa wakiunga mkono kila jambo linaloletwa
bungeni bila kutathmini matokeo ya sheria hizo kwa wananchi
wanaowawakilisha.
Alisema lazima ifike wakati wabunge wa CCM wabadilike na kuwatumikia wananchi wao.
“Nitakutana na wabunge wa CCM na kuwaambia kwamba sheria walizozipitisha
haziwasaidii wananchi… lazima chama kiwe na nguvu ya kuielekeza au
kuiwajibisha Serikali yake,” alisema Kinana huku akishangiliwa na
wananchi waliohudhuria mkutano huo.
Katibu Mkuu huyo alisema kuna haja ya kubadilisha mfumo wa utendaji kazi
wa chama na mojawapo ni kuchagua mtu mwingine wa kuongoza wabunge wa
CCM bungeni badala ya Waziri Mkuu kama ilivyo sasa.
Alisema Waziri Mkuu ataachwa atekeleze jukumu lake la kuiongoza Serikali
bungeni, lakini kuwe pia na kiongozi wa wabunge wa CCM bungeni. Alisema
mfumo huo utakipa chama nguvu zaidi ya kuisimamia Serikali yake.
“Wamekaa wabunge tena na kupitisha sheria ya kila gari kuwa na
kizimamoto, nani alisema gari langu lina mpango wa kuungua?” alihoji
kiongozi huku na kusema sheria nyingine zinatakiwa kufutwa kwa sababu
hazimsaidii mwananchi.
Aliishangaa Serikali ya CCM kwa kushindwa kufuta baadhi ya sheria ambazo
zimebainika kuleta usumbufu kwa wananchi na kusisitiza kuwa lazima
ifike wakati Serikali ifanye tathmini ya sheria zake na kuzifuta ambazo
hazifai kwa sasa.
“Nimekuwa waziri na kiongozi serikalini kwa muda mrefu, lakini sijawahi
kuona Serikali ikifuta sheria. Wamekuwa wakiongeza sheria mpya kila
siku. Hivi karibuni Serikali imepeleka miswada mingine 11 na yote
imepitishwa. Kwa namna hiyo tunambebesha mwananchi mzigo mkubwa,”
alisema.
Kinana aliitaka Serikali kuwashirikisha wananchi wakati wa kutunga
sheria ili kuondoa changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa
mara.
Kuhusu ahadi za Rais
Kinana alisema Serikali imefanya mambo mengi katika kuliletea Taifa
maendeleo kwa kutekeleza kikamilifu Ilani ya CCM ya mwaka 2010 na ahadi
nyingine zilizotolewa na Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za urais.
Alisema wakati Serikali ikiingia madarakani mwaka 2005, kulikuwa na
wanafunzi wa elimu ya juu 48,000 tu, lakini sasa wanafikia 200,000.
Aliongeza kuwa zaidi ya vijiji 1,000 vimeunganishwa na umeme.
“Katika kipindi cha miezi 26 ambayo tulikuwa tunatekeleza maazimio ya
mkutano mkuu wa mwaka 2012, nimejifunza mambo mengi. Nimeyajua matatizo
ya wananchi kwa karibu zaidi, lazima Serikali iwe sikivu,” alisema
Kinana.
Akimkaribisha Kinana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye
aliwataka Watanzania wasimame imara kukataa senti tanotano kutoka kwa
wanaotaka kununua uongozi ambao baadaye wanataka kurudisha fedha zao.
“Ndiyo maana tunakumbana na ‘skendo’ kibao, kesho Escrow, keshokutwa
Richmond, vyote hivi dawa yake moja, lazima tuzuie wanaotaka kununua
uongozi… na kama hiki ndicho wanachokitaka, safari hii tutazuia
wanaotaka kununua uongozi.
“Hatuwezi kuzunguka nchi nzima kusafisha chama halafu, wachache wanakaa
chini wanasema nitanunua hawa, halafu sita nitakuachia… watashika adabu
mwaka huu na hii itakuwa fundisho.
“Niko tayari kuliongoza jeshi la vijana kukataa biashara ya kununua
uongozi na matumizi mabaya ya fedha kwenye uchaguzi… haya ndiyo
yanayoharibu maadili ya nchi hii kwamba mtu anaamua yake na mwaka huu
Mungu atawalaani,” alisema Nape.
Nape aliwatahadharisha wananchi kuepuka siasa za ushabiki kwani wakati
wao (wananchi) wakiathirika, watu wachache ndiyo wanaonufaika. Alisema
CCM imejipanga kuja kivingine katika jitihada za kuwatumikia wananchi.
“Chama cha Mapinduzi hakiuzi uongozi. Natoa wito kwa wale wote
wanaofikiri kuwa wanaweza kufanya hivyo watambue mapema kwamba
haiwezekani,” alisema.
Akimpongeza Kinana kwa juhudi zake za kukiimarisha chama kwa kutoka
ofisini na kwenda kwa wananchi, Nape alisema ziara za katibu mkuu huyo
zimetumia miezi 26 na siku 18 katika mikoa 31 nchini.
alisema katika ziara hizo, ametembea umbali wa kilomita 193,574 huku
akizindua miradi 2,671 na kuingiza wanachama wapya 208,432 na kati yao,
38,934 walitoka Chadema.
Katika mkutano huo, Nape alimtambulisha mwimbaji mpya ambaye atarithi
mikoba ya marehemu John Komba kuongoza bendi ya TOT katika uhamasishaji
wa chama.
Alimtaja mrithi huyo kuwa ni Twalib Neka na kusema kuwa ameshakamilisha albamu yake ya kwanza akiwa na bendi hiyo.
Mwananchi
0 comments :
Post a Comment