Ukawa wawasha moto wa BVR Dar.

Monday, June 29, 2015

Nkupamah blog


Joto la uandikishaji wananchi katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa kutumia mashine Biometric Voters Registration (BVR) nchini, limezidi kupanda jijini Dar es Salaam baada ya vyama vya siasa kujitosa kutoa elimu kwa wananchi na wanachama.

Vyama hivyo vinavyoonekana kuwa mstari wa mbele kuhamasisha wanachama wake wajiandikishe kwenye daftari ni vile vilivyomo kwenye Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema, CUF na NCCR- Mageuzi na vingine visivyo kwenye umoja huo ACT- Wazalendo na CCM.

Viongozi wa vyama hivyo kwa nyakati tofauti wamekuwa wakihamasisha wanachama wao kujiandikisha kwenye daftari hilo ili waweze kupata haki ya kupiga kura kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee, alisema juzi jioni kuwa nguzo kuu ya kuingia Ikulu ni kupitia wanawake kwani endapo watajiandikisha kwa wingi, Ukawa wanaweza kuibuka na ushindi mnono.

Alisema kutokana na kutambua umuhimu wa wanawake kwenye uchaguzi ujao, Baraza la Wanawake Chadema Taifa (Bawacha), limeanzisha kampeni ya kuwahamasisha wanawake kujiandikisha kwa wingi kwenye daftari hilo ili siku ya uchaguzi waweze kupata haki ya kuwapigia kura wagombea wanaowataka.

Nayo Jumuiya ya Wanawake wa Chama cha Wananchi (CUF- Juce), Wilaya ya Ilala imeunda kikosi kazi cha watu 20 kuhamasisha wanawake wilaya hiyo kujitokeza kujiandikisha katika daftari hilo kazi hiyo itakapoanza jijini humo hivyo karibuni.

Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Ania Chaurembo, alisema kikosi hicho kimepanga kuhamasisha wanawake nyumba kwa nyumba, mtu mmoja mmoja na mtaa kwa mtaa.

Alisema lengo ni kuhakikisha wanawake wengi zaidi wanajitokeza kujiandikisha katika daftari hilo ili Oktoba 25 mwaka huu wamchague kiongozi bora kupitia Ukawa, ambaye wanaamini atakuwa suluhisho la matatizo yao ya muda mrefu.

Chaurembo alisema pamoja na kwamba wanawake ndiyo wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupiga kura, lakini wanaamini bado wapo baadhi yao wanashinda kushiriki kutokana na kutokujiandikisha katika daftari hilo.

Alisema kikosi kazi hicho kitahakikisha hakuna mwanamke anayebaki bila kujiandikisha kwa kuwa wanaamini elimu watakayoitoa itawasaidia hata wale baadhi yao waliokuwa wanashindwa kujiandikisha kwa kutofahamu haki yao ya kufanya hivyo.

Aliongeza kuwa kwa mwaka huu, idadi ya wanawake waliojitokeza kuwania nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho na Ukawa ni kubwa, hivyo upo umuhimu mkubwa kwa wengi wao kujiandikisha ili wawachague wanawake wenzao siku ikifika.

"Tunaamini kwamba changamoto mbalimbali zikiwamo za afya ya uzazi zitatatuliwa tukichagua viongozi wengi wanawake."
Aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuhakikisha inaandikisha wananchi wote katika maeneo iliyokwisha kufanya kazi hiyo ambao hawakuandikishwa kutokana na muda uliotolewa kuwa mdogo.

Wakati vyama vya siasa vikifanya jitihada hizo, baadhi ya wakazi wa Dar es Salaam wameilalamikia NEC kwa kupanga muda mchache wa uandikishaji katika daftari hilo kwa jiji hilo, wakidai utawafanya wengi wao kukosa haki ya upigaji kura katika uchaguzi mkuuOktoba mwaka huu. NEC ilitarajia kuandikisha wakazi milioni mbili wa Dar es Salaam katika BVR.
Mkuu wa Kitengo cha Teknolojia ya Habari na Mwasiliano (Tehama) NEC, Dk. Sisti Karia, alisema changamoto wanazokumabana nazo katika kila eneo la uandikishaji nchini, zimekuwa zikitatuliwa ikiwamo kuongeza siku kwa baadhi ya maeneo yenye foleni kubwa ya watu.

Alisema uandikishaji wa maeneo waliyokwisha kuandikisha umevuka malengo na kwamba litakuwapo dirisha dogo la uandikishaji kwa waliokosa fursa hiyo.

NEC juzi ilitoa taarifa ya kuahirisha uandikishaji kwenye daftari hilo jijini humo hadi tarehe nyingine itakayotangazwa .
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo habari, iliyotolewa na Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba, tume hiyo imeahirisha uandikishaji katika daftari hilo kutokana na kuchelewa vifa vya uboreshaji kutoka mikoani.

Vifaa vilivyokuwa vinakusudiwa kuanza kutumia jijini humo vimepelekwa katika mikoa ambayo wananchi wamejitokeza kwa idadi kubwa kujiandikisha kwenye daftari hilo.

Tume hiyo imetoa wito kwa wakazi wa jiji hilo kuwa watulivu wakati vifaa vikisubiriwa kutoka mikoani.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment