Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF, Magdalena Sakaya
akizungumza, Dar es Salaam jana kuhusu vikao vya Baraza kuu la uongozi
wa Chama hicho kwa ajili ya kutoa uamuzi wa kumsimamisha mgombea wa
nafasi ya Urais kupitia Umoja wa katiba ya Wananchi Ukawa. Kulia ni
Mkurugenzi wa Habari, Abdul Kambaya. Picha na Venance Nestory
Dar es Salaam. Baraza
Kuu la Uongozi wa Taifa la Chama cha Wananchi (CUF), limeutaka uongozi
wa chama hicho kusitisha uamuzi wa kumpata mgombea urais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kupitia vyama vinavyounda Ukawa hadi suala hilo
litakapojadiliwa kikatiba ndani ya chama hicho Julai 25.
Akizungumza na waandishi wa habari jana kwenye Ofisi Kuu ya chama hicho
Buguruni, Dar es Salaam, Naibu Katibu Mkuu Bara, Magdalena Sakaya
alisema wajumbe wa baraza hilo ndiyo wenye uamuzi wa kutoa tamko la
kuendelea kuwamo ndani ya Ukawa au kujitoa.
Taarifa hizo za CUF zinakwenda tofauti na taarifa iliyotolewa juzi na
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia kwamba wamekamilisha mazungumzo
ya kumpata mgombea wa urais ambaye atatangazwa kwenye mkutano wa
hadhara muda wowote ndani ya siku saba.
Mbatia, ambaye pia ni Mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi akizungumza akiwa na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel
Makaidi na viongozi wengine wa vyama hivyo, alisema hakuna mpasuko kama
inavyodaiwa na kusisitiza kwamba bado wapo na CUF katika umoja huo.
Hata hivyo, jana Sakaya alisema: ”Hili la kujiunga na Ukawa linatakiwa
kujadiliwa kwa kina na Baraza Kuu na hata ikiwezekana kuwashirikisha na
wanachama ndipo mwafaka wa kujiunga au la utolewe.”
Alisema hata baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba
kutangaza mbele ya viongozi wa Ukawa kwamba juzi wangemtangaza mgombea
wa urais lilikuwa ni kosa kwani liliwashtua wajumbe wa Baraza Kuu kwa
kuwa hawakushirikishwa.
Alisema kutokana na katiba ya chama hicho, hakuna kiongozi yeyote mwenye
mamlaka ya kutangaza jambo kama hilo hadharani bila ya kushirikisha
Baraza Kuu ili litoe baraka zake. Alisema jambo jingine ambalo
liliwashtua wajumbe wa baraza hilo na wanachama wao ni baada ya kusikia
taarifa mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii
kwamba tayari mgombea urais kupitia vyama vinavyounda Ukawa
ameshapatikana.
“Ni jambo la kushangaza kwani mpaka idadi ya kura ambazo mgombea huyo
kupitia chama fulani alizozipata zimewekwa hadharani kupitia vyombo vya
habari na mitandao ya kijamii, suala hili lilitushtua sisi viongozi na
hata wajumbe wa baraza Kuu hivyo tumeona tulijadili kwanza,” alisema.
Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Bunge wa CUF, Shaweji Mketo
alisema ni muhimu Watanzania wakatambua kwamba CUF haijajitoa Ukawa,
bali ni mchakato tu unaoendelea kwa mujibu wa sheria ya chama hicho.
Alisema nchi inapitia kipindi kigumu na pia ongezeko la majimbo 26 ya
uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika
kipindi kifupi kabla ya kuanza kwa kampeni, ni changamoto kubwa kwa
Ukawa.
Alisema CUF ina imani kwamba kwa maridhiano ya pamoja, Ukawa itajengwa
imara na hatimaye kuwa na mgombea mmoja wa urais, wabunge na madiwani.
Mbowe atoa ufafanuzi
Akizungumzia msimamo huo wa CUF, Freeman Mbowe alisema wamewaelewa
vizuri wenzao na kwamba masuala ya chama yanasimamiwa na viongozi, hivyo
ni lazima wayamalize kwa mchakato wao ndani ya chama ndipo
wajihakikishie ushiriki wao.
“Kuhusu hoja ya CUF kusikiliza Baraza lao Kuu kwanza ni suala la msingi
sana na wameshatwambia na tumewaelewa kwa sababu hata sisi tulipata
baraka zote ndani ya baraza ndiyo maana tukaamua kushiriki kikamilifu,’’
alisema.
Alisema ana imani kwamba CUF, itashiriki kikamilifu kwenye Ukawa
kuhakikisha wanampata mgombea mmoja kama walivyowaahidi wananchi.
“Wananchi wanatuamini sasa lazima haya mambo tuyafanye kwa umakini sana
ili tusije tukajiharibia sifa na kuambulia aibu kutoka kwa wananchi
ambao wana imani na sisi,’’ alisema.
MWANANCHI


0 comments :
Post a Comment