Mwenyekiti
wa Chadema, Freeman Mbowe (kulia) akifurahia jambo na wajumbe wa Kamati
Kuu ya chama hicho walipohudhuria kikao cha dharura katika Hoteli ya
Bahari Beach, jijini Dar es Salaam jana. kuanzia
kushoto ni Ezekia
Wenje, Mchungaji Peter Msigwa na Naibu Katibu wa chama hicho (Zanzibar),
Salum Mwalimu. Picha na Edwin Mjwahuzi.
Licha ya
Baraza Kuu la Uongozi la Chama cha Wananchi (CUF) kupokea taarifa ya
Ukawa na kuamua chama hicho kiendelee kushiriki katika umoja huo, bado
suala la mgombea urais wa vyama vinavyounda umoja huo limeendelea kuwa
siri nzito.
Taarifa
zilizopatikana kutoka ndani ya CUF jana, zilisema kuwa katika kikao
chake kilichoketi juzi na jana mjini Zanzibar, baraza hilo lilipokea
taarifa ya Ukawa, kuithibitisha na kuamua chama hicho kiendelee na
ushirikiano huo.
Mkutano wa waandishi wafutwa
Pamoja na
hayo, jana kutwa nzima viongozi wa Ukawa walikuwa kwenye vikao
mfululizo na hakukuwa na taarifa rasmi zilizopatikana na hata mkutano na
waandishi wa habari ulioitishwa jana jioni uliahirishwa bila kueleza
utaitishwa tena lini.(P.T)
Ingawa
taarifa ya mkutano wa Ukawa na wanahabari haikutaja ajenda, habari
zilizoenea katika mitandao ya kijamii zilibainisha kuwa walikuwa
wanakusudia ama kutangaza chama kilichopitishwa na Ukawa kusimamisha
mgombea urais au kutangaza jina la mgombea mwenyewe pamoja na mgombea
mwenza.
Vyanzo
mbalimbali ndani ya Ukawa, vilieleza kuwa ufunguo wa hatua hiyo ulikuwa
unashikiliwa na CUF, ambayo hivi karibuni ilijitenga na umoja huo ili
masuala yake yajadiliwe kwanza na vikao vyake vya maamuzi kabla ya
kurejea kwenye meza ya majadiliano.
Taarifa
za uhakika kutoka katika kikao hicho kilichoketi Zanzibar kwa siku
mbili, zilibainisha kuwa wajumbe waliafikiana kinyume na ilivyotarajiwa
kuwa wangevurugana.
Miongoni mwa mambo ambayo inadaiwa wameafikiana ni kuwa mgombea urais atoke Chadema na chama hicho kitoe mgombea mwenza.
Jussa: Watanzania mtafurahi
Hata
hivyo, mmoja wa wajumbe wa baraza hilo, Jussa Ismail Ladhu alipoulizwa
alisema ikiwa itaamuliwa mgombea mwenza wa Ukawa atoke CUF, hakutakuwa
na shida kwa kuwa chama hicho kina wanasiasa wazuri, safi na makini na
kwamba kitatoa mtu ambaye Watanzania wote watafurahi.
“Ikiamuliwa
kuwa mgombea mwenza atoke CUF, wananchi msiwe na wasiwasi, CUF ina
hazina nyingi, itatoa mtu bora, itawapa chaguo ambalo Watanzania wote
wataridhika nalo,” alisema Jussa.
Pamoja na
kuthibitisha kuwa Baraza hilo limeamua CUF iendelee kushiriki katika
umoja huo, Jussa alisema kwenye mjadala matatizo kidogo yalikuwapo
katika mgawanyo wa majimbo.
Hata
hivyo alisema baada ya kuweka vigezo vya kuwa na mgombea wa Ukawa, sasa
hakuna shida kwa kuwa majimbo machache yaliyosalia utaratibu wake
utatangazwa hivi karibuni.
Kuhusu
mgombea mwenza, Jussa alisema CUF ina nafasi kubwa ya kutoa mgombea huyo
kwa sababu ndicho chama chenye nguvu Zanzibar na kina wanasiasa mahiri
na makini.
Wagombea
wetu tunataka wawe ni wale watakaohakikisha kuwa Katiba Mpya inapatikana
mara baada ya uchaguzi ili kuyaweka sawa mambo yanayohitaji kuwekwa
sawa.
Hata
hivyo, kwa mujibu wa Katiba, mgombea urais na mgombea mwenza wanapaswa
kutoka chama kimoja, hivyo kama Chadema itamtoa mgombea urais inabidi
pia mgombea mwenza atoke chama hicho.
Habari ambazo bado si rasmi zinasema kuwa mmoja wa viongozi wa CUF anaweza kuhamia Chadema ili kukidhi matakwa hayo ya Katiba.
Mkurugenzi
wa Haki za Binadamu, Habari, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa CUF,
Salim Bimani alisema kuwa mambo katika Ukawa ni mazuri, wapo waliofikiri
kuwa watavurugana, lakini wamekubaliana na sasa Watanzania wasubiri
kupata wagombea safi katika ngazi zote.
Bimani alisema CUF kitaendelea kushirikiana na vyama vingine vya upinzani nchini ili kuhakikisha demokrasia inazidi kukua.
Vikao mfululizo Chadema
Habari
zaidi zilizolifikia gazeti hili zilisema mshirika mwingine wa Ukawa,
Chadema jana viongozi wake walikuwa katika kikao cha dharura cha Kamati
Kuu kilichoshirikisha wajumbe wachache, hasa wale wanaopatikana kwa
kupigiwa kura ili kuweka mambo sawa.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene alikiri kuwapo kwa kikao hicho.
“Kamati
Kuu ya Chadema inaendelea kukutana jijini Dar es Salaam kwa kikao
maalumu cha dharura kujadili mambo mbalimbali,” alisema Makene katika
taarifa yake fupi aliyotuma jana usiku.
“Mambo
hayo ni pamoja na maandalizi ya chama kuelekea uchaguzi mkuu, kupokea
taarifa za mwenendo wa kura za maoni na uteuzi wa awali wa nafasi za
ubunge wa majimbo na viti maalumu zinazoendelea nchini nzima,” alisema
Makene.
Habari za
ndani ya kikao hicho kilichofanyika katika Hoteli ya Bahari Beach
jijini Dar es Salaam, zilisema kuwa kilikuwa na jukumu la kupokea
taarifa ya utafiti iliyofanywa nchini kote kuhusu mgombea anayekubalika
zaidi.
Ingawa
hakukuwa na taarifa rasmi kuhusu utafiti huo, lakini taarifa
zinazoendelea kusambaa zinalitaja jina la waziri mkuu wa zamani, Edward
Lowassa kuwa yuko mbioni kuhama chama chake cha CCM na kwenda Chadema,
huku mgombea mwenza akitajwa kuwa atatoka upande wa Zanzibar CUF.
Mgombea mwenza kuhamia Chadema
Habari za
ndani ya Ukawa zinasema chini ya makubaliano ya Ukawa ikiwa mgombea
urais atatoka Chadema, mgombea mwenza akitoka chama kingine itabidi
ahame chama chake ili aingie chama alicho mgombea urais ili kukidhi
matakwa ya kikatiba.
“Tutakaposhinda
uchaguzi, kama makamu wa rais atatoka CUF itabidi kila akitoka katika
ofisi ya makamu wa rais, kituo cha kwanza atasimama Makao Makuu ya CUF
kwa ajili ya kupeleka taarifa na kupata baraka za chama katika masuala
muhimu.”
Chanzo
chetu cha habari kinasema: “Ikiwa Ukawa tutashinda Uchaguzi Mkuu Oktoba
25 na kupata nafasi ya urais, jambo la kwanza litakuwa ni kufanya
Mabadiliko ya Katiba na kuruhusu demokrasia pana ya watu kuungana.”
Alisema hakuna ajabu yoyote kwa rais kutoka chama kimoja na makamu wa rais kutoka chama kingine.
“Hilo
hata sasa linatendeka Zanzibar ambako Rais na Makamu wa Kwanza wa Rais
wanatoka vyama tofauti na hakuna matatizo yoyote katika utendaji wa
Serikali, kila mmoja anasimamia kwanza maslahi ya Taifa pili kuhakikisha
sera za chama chake zinatekelezwa,” kilieleza chanzo cha habari.
Lowassa atajwa
Hii ndiyo
ajenda ambayo imetawala mijadala kuhusu fununu za Lowassa kuhama CCM
kwenda Chadema ili kukamilisha safari yake ya matumaini.
Gazeti
hili linafahamu kuwa mazungumzo na Lowassa yamekwishafikia hatua nzuri
ingawa kulikuwa na viongozi wachache ndani ya Chadema waliokuwa
wameshikilia msimamo wa kumkataa lakini kutokana na presha iliyopo ndani
na nje ya chama wasingefua dafu.
Mtei amkaribisha
Huku
mjadala kuhusu Lowassa ukizidi kukolea, mwasisi wa Chadema, Edwin Mtei
amemkaribisha mwanasiasa huyo na makada wengine wa CCM kujiunga na chama
hicho kikuu cha upinzani.
Akizungumza
na Mwananchi jana, Mtei alisema kwa sasa Chadema na Ukawa wanahitaji
kura za kutosha kuing’oa CCM, hivyo hata kura ya mtu mmoja ni muhimu.
“Nimesikia
Lowassa anatajwa kutaka kujiunga na Chadema, mimi namkaribisha aje, si
yeye tu, aje na makada wengine wa CCM kwa kuwa tunapaswa kuimarisha
nguvu za kuiondoa CCM madarakani,” alisema.
Alisema
Chadema ni chama cha Watanzania wote hivyo hakiwezi kumfungia milango
Mtanzania mwenye sifa za kujiunga na chama hicho asijiunge.
Hata
hivyo, Mtei alisema makada hao wa CCM ambao wanataka kujiunga na Chadema
endapo watakuwa na nia ya kupata uongozi, wajue kuna vikao vya
kuwapitisha.
“Tunawakaribisha
Chadema makada wote wa CCM bila masharti na kama wana nia ya uongozi
Chadema ina vikao vya kupitia kulingana na sifa zao na vikao vitakuwa na
maamuzi ya mwisho,” alisema.
Akizungumzia uchaguzi mkuu ujao, alisema ana uhakika muungano wa upinzani ndio silaha kubwa ya kuing’oa CCM madarakani.
“Uchaguzi
uliopita Chadema tulishinda lakini tulichakachukuliwa lakini safari hii
kupitia Ukawa tumejipanga kuhakikisha upinzani tunashinda kwa kiasi
kikubwa,” alisema.
Alisema hadi sasa Chadema na ukawa kwa ujumla wake kuna viongozi wenye sifa ya kushinda urais na wanakubalika nchi nzima.


0 comments :
Post a Comment